Na Sophia Kingimali
Mwenyekiti wa Wakurugenzi Shirika la Bandari Zanzibar, Joseph Abdallah ametoa rai kwa watoa huduma mbalimbali ndani ya bahari kuhakikisha wanapata elimu ya matumizi sahihi ya bahari ili kusaidia kukuza na kuendeleza uchumi kupitia bahari lakini pia kuendelea kuimarishi ulinzi kwa watumiaji wa bahari hiyo.
Akizungumza leo Disemba 4,2024 wakati akifungua kongamano la tatu la kitaaluma (Convocation) amesema elimu kwa wanaofanya kazi kwenye maji ni muhimu na endelevu.
“Bahari husafirisha mizigo mikubwa kuliko eneo lolote hivyo wataalamu wanaofanya shughuli huko wanapaswa kuwa na elimu ya kutosha na wanabeba jukumu kubwa kwa sababu endapo uzembe ukitokea na meli kuzama ni hasara kubwa kwani mali nyingi hupotea kuliko hata gari lingeanguka,” amesema Abdallah.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa wahitimu wanaomaliza katika chuo hicho kuhakikisha wanatumika vizur katika kuendeleza sekta ya bahari ili iweze kufika mbali.
“Nitoe rai kwa hawa wanafunzi wanaohitimu hapa DMI tuweze kuwatumia vizuri ili kuiendeleza sekta yetu ya bahari lakini pia hata wanafunzi wanaotaka kujiendeleza kwa kozi mbalimbali ambazo zinatolewa tuwakaribishe sana mje mjiendeleze”,Amesema Abdallah.
Kwa upande wake mkuu wa chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo amesema kupitia jitihada mbalimbali zilizofanyika sasa chuo chao kinashuhudia ukuaji wa idadi ya wanafunzi kutoka wanafunzi 1500 miaka mitatu nyuma hadi wanafunzi 5,100 waliodahiliwa sasa.
Amesema hali hiyo imefanya chuo chao sasa kukabiliwa na uhaba wa madarasa ofisi na vitendea kazi vingine jambo ambalo liliwafanya kuanza kuangalia namna ya kupanuka zaidi.
“Tulianza kuangalia namna ya kupanuka zaidi kwa kutafuta eneo kimbiji ambako tunatarajia kujenga chuo cha bahari ambacho kitaendana na sifa ya kimataifa ya chuo chetu sambamba na maono tulionayo,” amesema Profesa Gurumo.
Amesema kujengwa kwa chuo hicho sasa itakuwa ni mwanzo wa mabaharia wa Tanzania kuingia katika meli za Umoja wa Ulaya tofauti na iivyo sasa.
“Tunataka kufikia viwango ambavyo havina ukomo ili vijana waweze kupata ajira sehemu mbalimbali ili wakuze uchumi wa nchi. Pia tumepanua wigo kwa kwenda Lindi na Mwanza na tunatafuta eneo visiwani Pemba ili tuweze kusogeza mafunzo visiwani Zanzibar,” amesema.
Ameongeza kuwa kukua kwa idadi ya wanafunzi ni ishara kuwa elimu ya masuala ya bahari inazidi kuwapa fursa vijana za kuchagua nini wanataka ili kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi.
“Hilo litaenda sambamba na kujibu kiu ya upatikanaji wa rasilimali watu wenye weredi ili kujenga wataalamu wa ndani ya nchi badala ya kusubiri wanaokuja wawekezaji kuja na wataalamu wao”,Amesema.