Meneja wa shirika la umeme Tanzania TANESCO mkoa wa Rukwa Mhandisi Nyanda BUSUMABU wakati akizungumza na Wakandarasi.
Mgeni rasmi katika kikao hicho ambaye ni Katibu Tawala wilaya ya Sumbawanga Gabriel Masinga wakati akizungumza na wakandarasi katika ukumbi wa mikutano wa Tanesco mkoa wa Rukwa.
Baadhi ya wakandarasi waliohudhuria katika kikao kazi hicho.
…………………
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Rukwa. Shirika la umeme Tanzania TANESCO mkoa wa Rukwa limewataka Wakandarasi kufanya majukumu yao kwa mujibu wa maelekezo ya sheria na taratibu zilizowekwa na kuacha tabia ya kushirikiana na vishoka kwani wao ni daraja kati ya wananchi na shirika hilo.
Meneja wa Tanesco mkoa wa Rukwa mhandisi Nyanda Busumabu amewasihi kuacha mara moja kuwadanganya wateja kwa kuwajazia fomu za kuomba kuwekewa umeme na shirika hilo.
Mhandisi Nyanda amesema hayo wakati wa kikao kazi kati ya wakandarasi ambao ni wadau wa shirika hilo leo Dec 4 katika ukumbi wa mikutano wa TANESCO mkoa wa Rukwa.
Amewasisitiza wakandarasi waepukane na vitendo vya rushwa jambo ambalo linadhoofisha juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani za kuhakikisha kila kijiji kinafikiwa na umeme.
Aidha amesema wakandarasi wamebeba taswira ya tanesco na serikali hivyo amewataka wafanye kazi kwa uaminifu mkubwa na hurudisha huduma bora kwa wananchi.
“TANESCO tuna lengo la kupunguza kero mbalimbali za wateja hivyo hatuwezi kukubali vishoka watuharibie mipango yetu ya kuwahudumia wateja wetu kwa viwango wanavyostahili.”
Ameongeza kuwa wakandarasi wanatakiwa kujitofautisha na vishoka ili kazi wanayoifanya ilete matokeo chanya kwao na jamii inayowazunguka.
Awali akizungumza na wakandarasi hao kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile Katibu Tawala wilayani humo Gabriel Masinga amewataka wakandarasi kusajili kampuni zao.
Masinga amesema uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa kazi ndio nguzo muhimu za kujipatia kipato halali kwa kuwaweka wazi gharama za malipo na kuhakikisha kuwa yanalipwa kwa mfumo wa control number na kutoa risiti za kielektoniki.
Naye mwakilishi kutoka baraza la watumiaji wa huduma za nishati na maji EWURA Ramadhani Kakende amesema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja kuwa kuna udanganyifu mkubwa kwa baadhi ya wakandarasi na kuwapa tahadhari ili kujiepusha na ubadhirifu huo.
Meneja wa TANESCO katika mji wa Kitanesco wa Laela Nuru Yanga ameshauri wakandarasi hao kutoa taarifa katika maeneo yao ya kiutendaji ili kuongeza ufanisi katika kazi zao.
Akitoa wasilisho la mada iliyoandaliwa ya Ushirikiano wa ufanisi na wakandarasi Huduma bora kwa kila mteja.
Afisa uhusiano na huduma kwa wateja TANESCO mkoa wa Rukwa Angeline Bidya amewataka wakandarasi kujisajiri na huduma ya NIKONEKTI ili kufanya kazi kidijitali na kupata taarifa sahihi za mteja na kwa muda muafaka.
“Ili kuingia kwenye Nikonekti ni muhimu kila mkandarasi akawa na leseni pamoja na taarifa sahihi za mteja na hatimaye kuwasilisha ombi la mteja katika shirika letu”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ukandarasi Filbert Mwanandenje anayemiliki Mwanandenje company Limited amesema analishukuru shirika hilo kwa kuwakutanisha pamoja wao kama wadau ambao lengo lao ni moja la kuhakikisha mteja anapata huduma sahihi bila usumbufu wowote.