Dar es Salaam.
Kampuni ya usambazaji na uuzaji wa huduma na bidhaa za nishati ya Puma Energy Tanzania imetwaa tuzo ya Kituo Bora cha Mafuta kinachofikika na kupatikana kwa urahisi zaidi Tanzania katika tuzo za Consumer Choice Awards Africa (CCAA) 2024 zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa The Super Dome – Masaki, jijini Dar es Salaam.
Kampuni hii inajivunia mtandao wake mpana wa vituo vya utoaji wa huduma na bidhaa za nishati kwa teknolojia ya kisasa na huduma kwa wateja ya hali ya juu. Mteja anapotembelea vituo vyake hupata zaidi ya huduma ya ujazaji wa mafuta kwasababu anaweza kufanya manunuzi ya mitungi ya Puma Gas, mahitaji mbalimbali ya nyumbani kupitia duka lililopo, ukaguzi wa gari, huduma ya uoshaji, ujazaji upepo matairi, pamoja na bidhaa bora za vilainishi ili kumfanya asikwame katika safari yake.
Kupitia uwekezaji wa upanuzi wa vituo vipya ili kuwafikia wateja na Watanzania nchini kote, Puma Energy Tanzania huhakikisha inawezesha jamii inapoendeshea shughuli na kutoa huduma zake. Kampuni huzingatia kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa eneo husika ili kupunguza changamoto ya ajira na kuiwezesha jamii kuchangia katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika tuzo hizo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo alikuwa mgeni rasmi.
Tuzo hiyo ya Kituo Bora cha Mafuta Kinachofikika na Kupatikana kwa Urahisi Zaidi nchini, ilipokelewa na Mkurungenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma M. Abdallah akiambatana na wafanyakazi kutoka idara mbalimbali za kampuni hiyo.
Consumer Choice Awards Africa (CCAA) ni tukio la kila mwaka la utoaji tuzo ambalo linalenga kutoa tuzo kwa makampuni, mashirika na taasisi katika barani Afrika katika sekta mbalimbali za uchumi kupitia maoni ya umma au wateja yanayokusanywa kwa mtindo wa kura za mtandaoni kupitia tovuti ya waandaaji. Tuzo hizi zilianzishwa mwaka 2019 jijini Dar es Salaam Tanzania lakini pia hufanyika katika nchi zingine kama vile Kenya, Malawi, na Afrika ya Kusini.
Tuzo za mwaka huu wa 2024 zilifanyika wiki iliyopita, tarehe 30 Novemba katika ukumbi wa The Super Dome Masaki, jijini Dar-es-salaam, Tanzania, na kuhudhuriwa na makampuni 500 zaidi ya na wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali Afrika walishiriki, pia wageni mashuhuri kama vile viongozi wakuu wa serikali walihudhuria.