……….…
Na Sixmund Begashe -Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ameendesha kikao kazi cha Wizara na Maafisa Wanyamapori wa Wilaya nchini (DGOs) Jijini Dodoma kwa lengo la kupata uwelewa wa pamoja wa Uhifadhi endelevu wa Maliasili pamoja na utatuzi wa changamoto zilizopo.
Akijibu baadhi ya hoja zilizojitokeza katika kikao hicho, CP. Wakulyamba ameagiza Viongozi wote wa Jeshi la Uhifadhi kuhakikisha linasimamia mahusiano mema kati ya Jeshi hilo na Maafisa Wanyamapori wa Wilaya ili kuongeza ufanisi katika shughuli za uhifadhi na kuchukua hatua kali kwa askari yeyote atakaye haribu mahusiano hayo.
“Maafisa wanyamapori wa wilaya ndio viungo namba moja katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa, nyara za serikali na kupambana na ujangili katika jamii zetu na kusaidia utatuzi wa migogoro inayojitokeza hivyo nilazima tuendelee kudumisha mahusiano haya mema.” Amesema CP. Wakulyamba
Aidha CP. Wakulyamba licha ya kuwapongeza Maafisa hao kwa kuudhuria kikao hicho, amewaahidi kuwa maoni yao yote waliyoyatoa Uongozi wa Wizara utayafanyia kazi kwa maslahi mapana ya Taifa.
CP. Wakulyamba ameongeza kuwa Wizara inathamini mchango wa Maafisa Wanyamapori hao, ndio maana inatoa kipaumbele katika kutatua changamo zinazowakabili kwa kua ndio maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda na kuthamini vivutio vya utalii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wanyamapori Wizara ya Maliasilia na Utalii Dkt. Alexander Lobora amesema maafisa Wanyamapori ni kiungo namba moja katika mapambana dhidi ya majagili hivyo ameahidi Idara anayoiongoza itaendelea kufanya kazi kwa karibu zaidi ili kufikia malengo ya Taifa katika uhifadhi endelevu.
Naye Katibu wa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya nchini Bw. Nicodemus Mombia, akiongea kwa niaba ya washiriki wa semina hiyo ameipongeza wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwakutanisha na maafisa hao kutoka Halmashauri nchini kupitia kikazo kazi hicho cha siku mbili ni jambo litakalo saidia kuongeza hari kubwa kwa watendaji hao pamoja na kusaidia kutatua changamoto zilizopo hususani za wanyamapori wakali na waharibifu.
Kikao kazi hicho Kilichofunguliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Bungeni hivi karibuni kama sehemu ya kudumisha mashirikiano na watendaji katika ngazi mbalimbali kwenye Uhifadhi endelevu wa Maliasili na Utatuzi wa Migogoro kati ya Wananchi na Wanyamapori wakali na waharibifu.