Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya na Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Profesa Joseph Nduguru akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 3, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kuwasilisha mada katika Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Maonesho (STICE 2024) linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 3, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kuwasilisha mada katika Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Maonesho (STICE 2024) linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 3, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kuwasilisha mada katika Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Maonesho (STICE 2024) linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Washiriki wa Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Maonesho (STICE 2024) wakifatilia mawasilisho ya mada mbalimbali katika kongamano hil0.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wametakiwa kuwekeza nguvu katika kufanya utafiti wa kilimo kinachotumia matumizi ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu jambo ambalo litasaidia kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuleta tija katika uchumi.
Akizungumza leo Disemba 3, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Maonesho (STICE 2024), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya na Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Profesa Joseph Nduguru, amesema kuwa matumizi ya teknolojia ya sayansi yanasaidia kuharakisha ugunduzi wa mbegu bora ikiwemo chai, mahindi pamoja mpunga.
Profesa Nduguru amesema kuwa teknolojia imesaidia sekta ya kilimo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kudhibiti wadudu wahalibifu katika mazao.
“Ili kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo unapaswa kuwekeza katika utafiti na kufanya kilimo kinachotumia matumizi ya sayansi na teknolojia, ubunifu na kuleta tija kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kufanya shuguli mbalimbali” amesema Profesa Nduguru.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei, amesema kuwa wapo katika mikakati ya kupunguza upotevu wa samaki ili kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha kwa mwananchi.
Dkt. Kimirei amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti waliofanya samaki wamekuwa wakipotea kwa asilimia 40, huku akifafanua kuwa wavuvi wakivua kilo 100 ya samaki, kilo 40 zinapotea kutokana na mazingira sio rafiki.
“Tunaendelea kuelimisha jamii kwani Wizara ya Mifugo na Uvuvi wametengeneza mikakati hadi kufikia mwaka 2030 wawe wamepunguza upotevu wa samaki ili kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha kwa mwananchi” amesema Dkt. Kimirei.
Akiwasilisha mada ya : Mchango wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya Nchi pamoja na kuchochea ubunifu kwenye Biotechnology, Mtaalam wa Masuala ya Usimamizi wa Maliasili, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Pius Sihanda, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Biotechnology kwani yana mchango mkubwa katika uchumi wa Duniani na Afrika pamoja na kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya Tabia ya Nchi.
Profesa Sihanda amesema kuwa matumizi biotechnology ya bado madogo tofauti na nchi zilizoendelea, huku akieleza kuwa hali hiyo inatokana na ukosefu wa teknolojia ya kutosha nchini kwa ajili ya matumizi ya biotechnology.
“Biotechnology inaweza kutumika katika maeneo mengi ikiwemo sekta ya afya na kilimo, hivyo ubunifu wa ziada unaitajika ili kuweza kutumia teknolojia kwa ajili ya kuleta manufaa kwa Taifa” amesema Profesa Sihanda.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, amehamasisha matumizi ya vyakula vya asili ambavyo vilikuwa vinatumika miaka ya nyuma kwa ajili kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya bora.
Kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Maonesho (STICE 2024) limebeba kauli mbiu isemayo: Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika kuimili changamoto za mabadiliko ya Tabia ya Nchi na kuchangia katika uchumi shindani.