Katibu tawala mkoa wa Rukwa Msalika Makungu wakati akizungumza na madaktari bingwa waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Sumbawanga
Baadhi ya madaktari bingwa waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Sumbawanga kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa
………………
Na Neema Mtuka Sumbawanga.
Rukwa. Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga Dr. Ismail Macha ametoa wito kwa wananchi wa mikoa ya kanda ya Magharibi kufika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa.
Dr Macha ametoa wito huo Leo Dec 2 2024 wakati akizungumza na madaktari bingwa waliofika kwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa .
Dr Macha amesema kuwa kuna madaktari Bingwa 32 wa fani 15 ambao watatoa huduma hizo za kibingwa na kila fani ina zaidi ya madaktari 2 mpaka 3 ambao wote kwa pamoja watatoa huduma hizo.
Ameendelea kwa kuwasisitiza wananchi kujitokeza na kuja kupata huduma za kibingwa ambazo walikuwa wakitembea umbali mrefu kuzifuata tena kwa gharama kubwa.
“Lengo letu ni kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi ambazo hapa katika hospitali yetu hakuna hivyo niwatake wananchi kujitokeza ili kupata huduma za afya pamoja na ushauri.”
Dr Macha pia amezitaja huduma za kibingwa zitakazotolewa na madaktari hao kuwa ni matatizo ya macho ,masikio, meno ,moyo, ngozi pua, koo ,mifupa ,magonjwa ya wanawake ,magonjwa ya watoto/utengamavu,afya ya akili ,upasuaji ,ganzi na usingizi na magonjwa ya ndani.
Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Charles Nyerere Katibu tawala wa mkoa wa Rukwa Msalika Makungu amewakaribisha madaktari hao na kuwataka kufanya kazi iliyowaleta kwa weredi mkubwa ili wananchi wanufaike na ubobezi wao.
Aidha amesisitiza kuwa na utamaduni wa kusogeza huduma kwa wananchi utaleta tija katika sekta ya afya.
“Nawapongeza kwa kukubali kuja Rukwa niwaombe tumieni taaluma zenu ili wananchi wanufaike”
Amesema huduma hizo za kibingwa zinawapunguzia wananchi gaharama za kusafiri umabli mrefu kuzifuata.
Awali akizungumza na madaktari hao mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile amesema ujio wa madaktari bingwa umeokoa zaidi ya sh mill 50 pesa ambazo wananchi hutoa pindi wanaposafiri kufuata huduma jijini Dar es salaama na Mbeya.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dr Ibrahimu Isaac amewasihi wananchi kuitumia vyema nafasi hii ya uwepo wa madaktari bingwa ili kupata huduma stahiki.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi akiwemo Anna Gilbert amesema kuwa ujio wa madaktari bingwa utawapunguzia gharama ya kusafiri umbali mrefu na kuzifuata huduma za kibingwa ambapo zamani walikuwa wakitumia gharama kubwa kuzipata.
“Naipongeza serikali kwa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi kwani gharama ambazo zimekuwa zikitumika kwa baadhi yetu ni kubwa hasa ukiambiwa uende nchini India ukafate matibabu huku unakata tamaa”.
Huduma za kibingwa zitatolewa kwa kanda ya Magharibi zikihusisha mikoa ya Katavi ,Kigoma ,Tabora na Rukwa Ambapo huduma hizo zimeanza kutolewa Leo tarehe 2 /12 /2024 hadi tarehe 6/ 12 /2024 katika hospitali ya Rufaa ya mkoa Sumbawanga.