Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mhandisi Victor Seff amewataka Mameneja wa TARURA wa Mikoa na Wilaya zote nchini kufanya ukaguzi na matengenezo ya Miundombinu ya barabara zinazosimamiwa na TARURA mara kwa mara ili kubaini kasoro na kuchukua hatua za haraka kuondoa kasoro hizo.
Kauli hiyo ameitoa wakati alipofanya kikao kazi na Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TARURA katika Ukumbi wa Odotorium, Millennium Tower – Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Seff ameonesha kutofurahishwa na hali ya matengenezo ya Miundombinu ya Barabara zinazosimamiwa na TARURA kufuatia ziara yake ya hivi karibuni aliyoifanya katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.
” Suala la matengenezo ya Miundombinu ya Barabara bado hatujafanya vizuri sana. Ukiona maeneo mengi bado hayafanyiwi matengenezo kwa wakati na haswa upande wa madaraja na mifereji ambayo tukikutwa na mvua yanaweza kutokea majanga ikiwemo miundombinu ya barabara kukatika na hata kupelekea maeneo mengine kutofikika kabisa.”
” Kwa hiyo leo tunakumbushana kuhusiana na hilo ili tuwe makini kuanzia kwenye upangaji (planning) mpaka kwenye utekelezaji ili kuhakikisha kwamba tunafanya matengenezo kwa wakati kuzuia barabara kukatika hata yale maeneo ambayo tungeweza kuyaokoa kabla mvua hazijaanza kunyesha.” Amefafanua
Mhandisi Seff aliwaasa Mameneja hao kuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye miundombinu ya barabara na kama watagundua kasoro wanapaswa kuandaa taarifa na kuiwasilisha Makao Makuu ili hatua za haraka za marekebisho ya kasoro hizo ziweze kuchukuliwa.
” Shida sio mvua ila shida ni je tunafanya kazi zetu kama tunavyotakiwa?”
“Tusisubiri mpaka madaraja yavunjike ndio tunakimbilia kuomba hela za dharura. Tutimize kwanza jukumu letu halafu kama ikitokea mvua ni nyingi kweli na sio tunasingizia mvua zilikuwa kubwa kumbe sisi wenyewe hatukufanya matengenezo yaliyopaswa kwa wakati muafaka.”
Amesema suala la matengenezo ya Miundombinu ya barabara lazima tulipe umuhimu wa hali ya juu kabisa haswa kwa madaraja na barabara mpya ambazo zimejengwa ili tuweze kutambua muda ambao umesanifiwa uweze kufikiwa kama ubunifu (designing) inavyosema.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala Bi. Azimina Mbilinyi aliwashukuru Mameneja hao kwa kazi wanazoendelea kuzifanya pamoja na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo na kuwaasa kuendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba wanabaki katika mstari.