Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma kushiriki kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani leo tarehe 01 Desemba 2024. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Dkt. Jerome Kamwela wakati akitembelea mabanda ya maonesho katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 01 Desemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa viongozi wa Baraza la Watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (NACOPHA) wakati akitembelea mabanda ya maonesho katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 01 Desemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati akitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho katika kushiriki kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 01 Desemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa uzinduzi na kukabidhi magari na pikipiki za kutoa huduma za chanjo katika Halmashauri mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 01 Desemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhi mfano wa funguo ya gari kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas kwa niaba ya wakuu wa Mikoa mingine mara baada ya kuzindua magari na pikipiki za kutoa huduma za chanjo katika Halmashauri mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 01 Desemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipokea maandamano ya vikundi mbalimbali vikiingia Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani tarehe 01 Desemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 01 Desemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Mpango wa Kwanza wa Uendelevu wa Mwitikio wa VVU na UKIMWI Tanzania Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera , Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa mara baada ya kuzindua mpango huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma tarehe 01 Desemba 2024.
………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta, wadau na jamii kwa ujumla kuweka mkazo katika kudhibiti mazingira yanayochochea maambukizi ya UKIMWI.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma. Aidha, ametoa wito kwa vijana kujitambua, kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa kasi ya maambukizi katika kundi la vijana bado inaonekana kuwa kubwa ambapo takwimu za hali ya UKIMWI nchini zinaonesha kundi la vijana na hasa wa kike liko kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi mapya ya VVU.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi kuzingatia maudhui ya elimu inayotolewa kupitia kampeni mbalimbali kwa ajili ya kubadili tabia, kuachana na mila zinazoweza kuwa vichocheo vya maambukizi na kuendelea kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI. Amesema hali ya maambukizi mapya inaonekana kuchochewa zaidi na mazingira na tabia hatarishi hususan ulevi uliopindukia, ngono zembe, kuwa na wapenzi wengi na matumizi ya dawa za kulevya.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuondoa mtazamo hasi uliopo juu ya walioathirika ambao huchangia kurudisha nyuma jitihada za kupambana na UKIMWI. Amesema mtazamo hasi huwafanya wahitaji kushindwa kupata huduma kwa kuonekana kuwa hawastahili na hivyo kutengwa. Ameongeza kwamba unyanyapaa hupelekea woga unaoathiri upimaji kwa hiari na upatikanaji wa huduma nyingine kama za unasihi pamoja na ARV kwa wale wanaoishi na VVU.
Amesema mapambano dhidi ya UKIMWI yaliyoanza takriban miongo minne iliyopita, yamepata mafanikio ambapo matokeo ya utafiti wa viashiria vya VVU na UKIMWI uliofanyika mwaka 2022/23, yanaonesha kuwa maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri kuanzia miaka 15 ni watu 60,000 kwa mwaka. Aidha, kiwango cha ushamiri wa VVU kitaifa ni 4.4% ambapo jumla ya watu 1,548,000 wanaishi na VVU.
Kiwango cha ushamiri wa VVU kwa wenye umri kuanzia miaka 15 na zaidi kwa upande wa Tanzania Bara ni 4.5% na 0.4% kwa upande wa Zanzibar. Viwango vya ushamiri kwa mikoa ya Tanzania Bara vinaanzia 1.7% (Kigoma) hadi 12.7% (Njombe). Mikoa mitatu ya Mbeya, Iringa na Njombe ina viwango vya ushamiri zaidi ya 9% ambayo ni mara mbili ya kiwango cha Kitaifa.
Makamu wa Rais amesema mafanikio yaliyopo katika mapambano dhidi ya UKIMWI yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi. ametoa shukrani za Serikali kwa Mfuko wa Dunia (Global Fund), Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR) na Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kwenye utekelezaji wa afua mbalimbali za VVU na UKIMWI.
Katika maadhimisho hayo yamekabidhiwa magari 96 na pikipiki 300, vyenye thamani ya billioni 8 kwa ajili ya kuimarisha huduma za chanjo katika halmashauri hapa nchini. Makamu wa Rais ameishukuru Global Alliance for Vaccine and Iniatives (GAVI) kwa ufadhili wa magari hayo ambayo kwa kiasi kikubwa utaboresha huduma za chanjo na kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa yanayozuilika.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kutekeleza awamu ya tatu ya Mradi wa TIMIZA MALENGO ambao unaolenga Wasichana Balehe na Wanawake Vijana, wenye lengo la kuwasaidia kiuchumi na kijamii, ili kupunguza hatari na kuhakikisha wanabaki salama dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri 42”.
Amesema mradi mwingine ni DREAMS, yaani Determined, Resilient, Empowered, AIDS-free, Mentored, and Safe, ambao unalenga kupunguza maambukizi ya VVU kwa Wasichana balehe na Wanawake vijana, na unatekelezwa katika Halmashauri 14 nchini.
Awali Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Wizara itaendelea kufanya maboresho ya kuhakikisha maamuzi ya kuunganisha mwitikio kwa kujumlisha uratibu wa magonjwa ya ngono, homa ya ini na UKIMWI kama vihatarishi vinavyofanana na vinavyofananishwa katika njia za maambukizi, kwa pamoja vinawekewa mkakati madhubuti wa kupambana navyo ili kuimarisha afya za Watanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI Bi. Letcia Morris ametoa wito kwa Watanzania wote kuondosha changamoto zinazorudisha nyuma juhudi za serikali katika kukabiliana na UKIMWI ikiwemo unyanyapaa pamoja na kuacha kutumia dawa. Amesema Baraza hilo limeendelea kuimarisha jitihada kwa kuhakikisha makundi yote yenye mahitaji maalum yanafikiwa na huduma kwa namna ya kipekee.
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI kwa mwaka 2024 yanabeba Kaulimbiu isemayo “Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI”, ambayo inatoa msukumo kwa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika kupambana na maambukizi mapya, huduma kwa walioathirika na matunzo kwa yatima na watoto waliozaliwa na maambukizi.