Meneja wa Chama kikuu chaUshirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Marcelino Mrope,akitangaza bei ya korosho kwa wakulima wa zao hilo katika mnada wa sita uliofanyika katika Chama cha msingi cha Ushirika cha Naluale kijiji cha Chingulungulu ambapo bei ya wastani ilikuwa Sh.2,863 kwa kilo.
Baadhi ya wakulima wa korosho wa kijiji cha Chingulungulu wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wakiangalia bei ya zao hilo kupitia kompyuta mpakato wakati wa mnada wa sita uliofanyika katika kijiji hicho ambao bei ilikuwa Sh.2,863.
Makamu Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Kaisi Makolela,akizungumza na wakulima wa korosho wa kijiji cha Chingulungulu baada ya kukamilika kwa mnada wa sita wa zao hilo ambapo bei ya wastani ilikuwa Sh.2.863 kwa kilo moja.
……….
Na Mwandishi Maalum, Tunduru
TANI zaidi ya 2,878 za korosho ghafi, zimeuzwa na wakulima wa zao hilo katika mnada wa sita uliofanyika katika chama cha msingi cha ushirika Naluale kijiji cha Chingulungulu wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.
Meneja Mkuu wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru (Tamcu)Marcelino Mrope alisema,katika mnada huo bei ya chini ilikuwa Sh. 2,830 bei ya juu Sh.2,910 na bei ya wastani ni Sh.2,863 kwa kilo moja.
Amewashukuru wakulima wa kijiji cha Chingulungulu kwa niaba ya wakulima wengine wanaohudumiwa na chama hicho, kukubali kuuza korosho kwa bei ya Sh.2,863 wakati huu ambao minada ya korosho inaelekea kufika mwishoni.
Mrope,amewataka kuhakikisha wanafufua akaunti zao na majina yaliyopo kwenye akaunti hizo yanakuwa sahihi na kubakisha kiasi cha fedha ili kuepuka kaunti kufa jambo linaloweza kuwaletea usumbufu na kuchelewesha malipo ya fedha.
Katika hatua nyingine Mrope,amewasisitiza wakulima kuzingatia ushauri wanaopewa na maafisa ugani wakati wa maandalizi ya korosho kabla ya kufikishwa kwenye vyama vya msingi vya ushirika ili kupata korosho bora zitakazokubali na wanunuzi na kupata bei nzuri.
Kwa upande wake meneja wa bodi ya korosho tawi la Tunduru Shauri Mokiwa alisema,wakulima wa korosho wa wilaya ya Tunduru wanabahati kubwa kwa kupata bei nzuri ikilinganisha na msimu uliopita ambapo katika mnada wa kwanza bei ilikuwa Sh.1,900 kwa kilo moja.
Mokiwa alieleza kuwa,makisio ya uzalishaji wa korosho hapa nchini ulikuwa kati ya tani laki mbili hadi tatu lakini uzalishaji katika msimu wa kilimo 2023/2024 unaweza kuongeza hadi kufikia tani laki nne.
Mokiwa, amewataka wakulima kukatua au kuweka matuta kwenye mashamba yao ili kuhifadhi maji ambayo ni muhimu kwa ajili ya miti ya korosho hasa wakati wa kiangazi ambapo mvua zinakuwa zimemalizika.
Amewakumbusha kujiandaa na msimu mpya wa kilimo kwa kuweka akiba ya fedha kwa ajili kununulia pembejeo kwa kuwa pembejeo zinazotolewa bure na Serikali hazitoshelezi mahitaji yao kutokana na mahitaji kuwa makubwa.
Mmoja wa wakulima wa kijiji hicho Hamis Mitao,ameipongeza Serikali kwa kuendelea kusimamia bei ya zao la korosho,hata hivyo amewaomba wanunuzi kuongeza fedha zaidi ili waweze kukidhi mahitaji na gharama za kilimo cha zao hilo.