Na Neema Mtuka ,Sumbawanga
Rukwa. Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga Dr. Ismail Macha ametoa wito kwa wananchi wa mikoa ya kanda ya Magharibi kufika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa.
Dr. Macha ametoa wito huo leo Dec 1 2024 ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa madaktari bingwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa Sumbawanga.
Amesema kuwa kuna madaktari Bingwa 40 wa fani 15 ambao watatoa huduma hizo za kibingwa na kila fani ina zaidi ya madaktari 2 mpaka 3 ambao wote kwa pamoja watatoa huduma hizo.
Amesema ujio wa madaktari hao ni neema kwa wananchi kwa kuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan analengo la kuwafikishia wananchi wote huduma hizo za kibingwa.
Madaktari hao Bingwa wa mama Samia watatoa huduma za kibingwa kwa Kanda ya Magharibi na kuwataka wananchi kujitokeza ili kupata huduma hizo.
Ameendelea kwa kuwasisitiza wananchi kujitokeza na kuja kupata huduma za kibingwa ambazo walikuwa wakitembea umbali mrefu kuzifuata tena kwa gharama kubwa.
“Lengo letu ni kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi ambazo hapa katika hospitali yetu hakuna hivyo niwatake wananchi kujitokeza ili kupata huduma za afya pamoja na ushauri.”
Dr Macha pia amezitaja huduma za kibingwa zitakazotolewa na madaktari hao kuwa ni matatizo ya macho ,masikio, meno ,moyo, ngozi pua, koo ,mifupa ,magonjwa ya wanawake ,magonjwa ya watoto/utengamavu,afya ya akili ,upasuaji ,ganzi na usingizi na magonjwa ya ndani.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi akiwemo Silvia Maoni amesema kuwa ujio wa madaktari bingwa utawapunguzia gharama ya kusafiri umbali mrefu na kuzifuata huduma za kibingwa ambapo zamani walikuwa wakitumia gharama kubwa kuzipata.
“Naipongeza serikali kwa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi kwani gharama ambazo zimekuwa zikitumika kwa baadhi yetu ni kubwa hasa ukiambiwa uende nchini India ukafate matibabu huku unakata tamaa”.
Huduma za kibingwa zitatolewa kwa kanda ya Magharibi zikihusisha mikoa ya Katavi Kigoma Tabora na Rukwa kuanzia terehe 2 /12 /2024 hadi tarehe 6/ 12 /2024 katika hospitali ya Rufaa ya mkoa Sumbawanga.