Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .TUME huru ya Taifa ya uchaguzi imekutana na wadau wa uchaguzi mkoani Arusha kwa lengo la kupeana taarifa mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya kuanza kwa zoezi la uboreshaji wa daftari.
Akizungumza mkoani Arusha na wadau hao Jaji (rufaa) Jacobs Mwambegele amesema kuwa,maandalizi hayo pamoja na mambo mengine yanajumuisha uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura, uboreshaji wa majaribio,ununuzi wa vifaa na ushirikishwaji wa wadau.
Amesema kuwa, kufanikiwa kwa zoezi lolote kunatokana na ushiriki wa wadau ,hivyo ni matarajio ya Tume kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili lifanyike kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa.
Ameongeza kuwa, Tume kwa sasa inafanya maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura utakaoanza desemba 11 hadi 17 mwaka huu na utajumuisha mikoa ya Arusha,Kilimanjaro, na mkoa wa Dodoma kwenye halmashauri za wilaya ya Kondoa ,Chemba na mji wa Kondoa ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
“Sote tunafahamu kwa mujibu wa ibara ya 74 (6) ya katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ,Tume imepewa mamlaka ya kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge wa jamhuri ya Muungano na madiwani kwa Tanzania bara. “amesema .
Jaji Mwambegele amefafanua kuwa,Tume inaendelea na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambapo uzinduzi wake ulifanyika mkoani Kigoma .
Aidha uzinduzi huo ulienda sambamba na kuanza kwa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma,Tabora,na Katavi na kufuatiwa na Geita,Kagera,Mwanza,Shinyanga,Mara,Simiyu,Manyara,Dodoma ,Singida na Zanzibar.
Amefafanua kuwa , katika kuhakikisha Tume inaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha zoezi hili ,imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao kwa mara ya kwanza utamwezesha mpiga kura aliyepo kwenye daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia aina yoyote ya simu ya kiganjani au kompyuta.
Ameongeza kuwa,lengo la kuwakutanisha wadau hao mbalimbali ni kuwapa taarifa za uwepo wa zoezi hilo na kuwapitisha katika vifaa vitakavyotumika,mifumo ya uandikishaji itakavyoendeshwa na namna zoezi litakavyoendeshwa.
Naye Mkurugenzi wa uchaguzi ,akitoa mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura awamu ya kwanza kwa wadau amesema kuwa,Tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais na wabunge katika Jamhuri ya Muungano pamoja na madiwani kwa upande wa Tanzania Bara.
Amesema kuwa, kwa sasa wapo kwenye maandalizi kwa ajili ya kuanza zoezi hilo katika mkoa wa Arusha,Kilimanjaro na Dodoma kwenye halmashauri ya mji Kondoa na halmashauri za wilaya za Kondoa ,Chemba Kondoa ambapo zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura na zoezi litakamilika machi,2025.
“Kwa kuzingatia matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 wapiga kura 5,586,433 wapya wanatarajiwa kuandikishwa sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20 ,wapiga kura 4,369,531 inatarajiwa wataboresha taarifa zao .
Ameongeza kuwa,Tume imeridhia kufanyika kwa mabadiliko ya idadi ya vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka vituo 40,126 hadi kufikia vituo 40,170 kwa kurejesha vituo 44 vya kata 11 za halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro vya kuandikisha wapiga kura nchini ambavyo vitatumika katika.uboreshaji wa daftari 2024/25 ambapo vituo 39,753 vipo Tanzania bara na 417 vipo Zanzibar.
“Kwa mkoa wa Arusha kuna vituo 1,454 vitakavyotumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 86 katika vituo 1,368 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwak 2019/20.
Aidha kauli.mbiu inasema kuwa,”kujiandiksha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora ,kajiandikishe sasa.”.