Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Novemba 30, 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali kupitia wizara ya elimu itaangalia namna ya kuchangia maendeleo ya miundombinu ya Shule ya Msingi Pangani, Kibaha Mjini, mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kushiriki pamoja na wananchi na viongozi kwenye mbio za Coast City Marathon zilizolenga kuchangia miundombinu ya shule hiyo, Prof. Mkenda alieleza kuwa mkoa wa Pwani umeonyesha juhudi kubwa, na wizara itaendelea kuunga mkono jitihada hizo.
“Licha ya mpango wa Serikali wa elimu bila malipo, wadau na jamii hawakatazwi kushirikiana na Serikali kuboresha sekta ya elimu,” alisema Prof. Mkenda.
Aidha, alieleza kuwa ilikuwa ni wajibu wake kushiriki mbio hizo kwa sababu lengo lake limegusa moja kwa moja wizara anayoiongoza.
“Marathon hizi zikifanyika tena mwaka ujao na mkiniita kama mgeni rasmi, naahidi kushiriki kwa moyo wote kwa kuwa mimi ni mdau mkubwa wa michezo,” aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta, alisema mbio hizo zimechangia si tu kukuza sekta ya michezo bali pia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
“Michezo ni muhimu kwa afya na pia huchochea maendeleo ya vipaji. Kupitia mbio hizi, tumeshiriki kwa vitendo katika kuboresha miundombinu ya elimu,” alisema Mchatta.
Awali, Mwenyekiti wa Coast City Marathon, Dkt. Frank Muhamba, aliwashukuru Taasisi zilizoungana nao katika mbio hizo, akiwemo NHIF, TANESCO, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), CRDB, Hospitali ya Tumbi, na Wakala wa Misitu (TFS).
Mbio za Coast City Marathon zilihusisha umbali wa kilomita 5, kilomita 10, kilomita 15, na kilomita 21, huku watoto wakishiriki mbio za kilomita 2.5.