Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Pendo Mangali wakati akizungumza na viongozi waliochaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao wamekula kiapo hii leo
………………..
Na Neema Mtuka
Rukwa.Viongozi walioapishwa baada ya kutangazwa na wasimamizi wa vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika November 27 wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria.
Hayo yamesemwa na Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Sumbawanga wakati wa zoezi la kuwaapisha viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa November 27 mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya viongozi hao kula kiapo Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Sumbawanga Pendo Mangali amesema viongozi waliochaguliwa wanasimama badala ya Serikali katika maeneo yao.
Mangali amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa weredi na kuhakikisha wanasimamia 4R za Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
“Ninyi ni Serikali kuweni waadilifu na kusimamia rasilimali za nchi zisipotee.
Awali akiwaapisha viongozi hao Hakimu mkazi wa Wilaya ya Sumbawanga Patrick Julius Lipiki amesema kiapo hicho kinawataka kwenda kuwatumikia wananchi kwa weledi mkubwa na kwa kufuata sheria.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Pendo Mangali amewapongeza wenyeviti hao kwa ushindi na kuwataka kwenda kuwatumikia wananchi kama yalivyo matarajio yao.
Baadhi ya Wenyeviti wa mitaa na Wajumbe akiwemo Stella Sakale ,Raymond Katumbaku na Consolata Kauzeni wameahidi kwenda kufanyakazi ya kuwatumikia wananchi kwa weledi mkubwa na kukamilisha miradi iliyopo.
Kwa upande wao wananchi Mkoani Rukwa akiwemo Edwin Mwang’anga na Elizabeth Simsozwa wamewataka viongozi hao kwenda kufanya kazi mara mbili ya kazi zilizofanyika katika kipindi kilichopita kwani wana matarajio makubwa.
Kamanda wa Polisi wilaya ya Sumbawanga SP Michael Chimkonda amesema zoezi la Uchaguzi lilikwenda vizuri na kwa ambaye hajaridhishwa na Matokeo anapaswa kufuata sheria na sio Kufanya Vurugu.
Kwa upande wake afisa uchaguzi Manispaa ya Sumbawanga Hashimu Kilushwa amewataka viongozi hao kuwatumikia wananchi na kushirikiana nao katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mangali amewataka viongozi hao kuwa walinzi wa amani katika maeneo yaliyowazunguka na kuwahudumia wananchi bila upendeleo.
Jumla ya mitaa 165 ,vijiji 339 na vitongoji 1816 vimechukuliwa na chama cha mapinduzi (CCM) Ambapo baada ya zoezi la kupiga kura vyama vya upinzani vilivyosimamisha wagombea wake wametangazwa kuwa washindi katika mitaa 6.