Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo, Dkt.Gerald Ndika akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha ,Ilvin Mugeta akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Arusha kuhusu Maandalizi ya Mkutano huo.
……
Happy Lazaro, Arusha
Rais wa jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano na mkutano mkuu wa 21 wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Afrika Mashariki (EAMJA) utakaofanyika desemba 2 hadi 7 mkoani Arusha .
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha kuhusu maandalizi hayo ,Jaji wa Mahakama ya rufani na Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo,Dkt.Gerald Ndika amesema kuwa maandalizi ya mkutano huo tayari yamekamilika na Rais Samia atafungua mkutano huo rasmi desemba 3,na wanatarajiwa kushiriki majaji na mahakimu zaidi ya mia tatu kutoka nchi za Afrika mashariki.
Amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto , mafanikio pamoja na utendaji kazi wao katika nchi hizo sambamba na kupata uzoefu namna ya utendaji kazi yao na kupeana uzoefu .
Dkt.Ndika amesema kuwa ,chama hicho ni chama huru na malengo mkubwa ni kuhakikisha kunakuwa na utawala bora wa sheria katika nchi hizo sambamba na kutetea maslahi ya wanachama .
Amesema kuwa, chama hicho kina jukumu kubwa la kutetea na kulinda uhuru wa mahakama zetu kwani wanataka kuona nchi zetu zinakuwa na uhuru wa utawala wa sheria.
Ameongeza kuwa ,mkutano huo umekuwa na mwitikio mkubwa sana kutoka kwa majaji na mahakimu hao huku kauli mbiu ya mkutano huo ikiwa ni “uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki.kwa ajili ya kuimarisha utengamano na ukuzaji uchumi katika ukanda wa Afrika mashariki .
Amesema kuwa katika mkutano huo ataweza kujadili mada mbalimbali ikiwemo utendaji kazi katika eneo la utoaji haki kwani wanataka kuhakikisha maamuzi yanayotolewa yanakidhi ubora sambamba na kuangalia mafanikio mbalimbali.
Aidha amefafanua zaidi kuwa, watajadili pia mada kuhusu programu za maboresho ya mifumo ya utoaji haki jinai pamoja ja utendaji kazi wake kwa ujumla .
Dkt.Ndika amefafanua zaidi kuwa, watajadili mada kuhusu uboreshaji utoaji haki katika migogoro ya kazi kwa watu wengi kwani wengi wao wamejikuta wanaingia kwenye migogoro ya kazi ,hivyo wataangalia sheria za kazi na kuweza kutoa maamuzi ya pamoja.
“Mbali na hayo pia tunaweza kujadili matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuongeza ufanisi katika.utoaji haki katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na wenzetu wataweza kutueleza walipofikia pia na katika swala hilo la matumizi ya teknolojia Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa sana kwenye eneo hilo kwani sasa hivi wanafanya usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao jambo ambalo ni mafanikio makubwa sana .”amesema .
Ameongeza kuwa,desemba 5 utakuwa ni mkutano Mkuu wa uchaguzi wa majaji na mahakimu wa Afrika Mashariki ambapo watakuwa na kikao kwa ajili ya kuchagua viongozi wao watakaowaongoza kwa miaka ijayo.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Arusha ,Ilvin Mugeta amesema kuwa ,chama kimepewa jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mwaka huu kwani mkutano huo ulifanyika nchini Uganda mwaka jana ambapo kwa mwakani mwenyeji atakuwa ni Kenya.