Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari ameshiriki zoezi la upigaji wa kura kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika nchi nzima tarehe 27 Novemba 2024.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amepiga Kura katika Kata ya Ipagala Kituo cha Mbuyuni, Ilazo Jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kupiga kura Mwanasheria Mkuu wa Serikali amefurahishwa na kuridhishwa na mazingira ya kituo hicho na zoezi zima la upigaji wa kura linavyoendeshwa, ambapo amesema utaratibu wa upigaji wa kura umekuwa rahisi, na huku akiwasifu wasimamizi wa uchaguzi huo kwa kutoa maelekezo vizuri kwa wapiga kura.
“Nimetoka kutekeleza haki yangu ya kikatiba kwa kupiga kura kuwachagua viongozi wetu wa serikali za mitaa, hali ya kituo iko shwari na zoezi limekuwa rahisi imenichukua muda mchache kutekeleza haki yangu ya kupiga kura.”
Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika hatua nyingine Mhe. Johari amewapongeza Waandaji na Wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa namna wanaevyoendesha zoezi la upigaji wa kura hivyo kuwarahisishia wananchi kutekeleza haki yao ya msingi.
“Nawapongeza sana Waandaji na Serikali kwa ujumla wananchi wanaweza kutekeleza haki yao hii kwa urahisi kabisa”. Amesema Mhe. Johari
Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kupiga kura ikiwa ni sehemu ya haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
“Utaratibu safari hii umeboreshwa sana na hata utoaji wa elimu kabla ya kupiga kura umeweka vizuri, hivyo niwasisitizie wananchi wenzangu kujitokeza kwa wingi kutimiza haki ya kupiga kura.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Zoezi la upigaji wa kura kuwachagua Viongozi wa Serikali za Mitaa linaendelea nchi nzima ambapo wananchi wamejitokeza kwenye maeneo mbalimbali kutekeleza haki yao ya msingi kikatiba ya kuwachagua Viongozi wao wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji.