Mwamvua Mwinyi,Pwani
Novemba 26,2024
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amehitimisha kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkoa wa Pwani na kuwaasa wananchi kuwapigia kura wagombea wanaotokea Chama Cha Mapinduzi CCM.
Aidha amesisitiza kuwa uchaguzi huo utakuwa wa amani huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Akizungumza katika mkutano wa uliofanyika Novemba 26,2024 katika eneo la standi ya zamani ya Mabasi Maili Moja, wilayani Kibaha, Abdulla aliwahimiza wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwani ni haki Yao ya kimsingi.
“Naomba wananchi wote wa Mkoa wa Pwani mjitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura, Hakikisheni kila mmoja anamhamasisha mwenzake.
Maandalizi yaanze tulale mapema ili ikifika Novemba 27 tupige kura mapema,” alisema Abdulla.
Abdulla alieleza kuwa kuchagua viongozi wa CCM ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi, akisema kuwa chama hicho kina sera madhubuti na viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo. “
“Ukitaka kujenga nyumba imara, unahitaji msingi bora,Viongozi wa CCM ndio msingi wa maendeleo endelevu kwa wananchi,” aliongeza.
Alitoa wito kwa wananchi kujenga mshikamano wa kisiasa kwa kuchagua viongozi wenye nia ya dhati ya kuimarisha ustawi wa jamii na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Maili Moja, Ramadhani Lutambi alihamasisha wananchi kuichagua CCM ili kuhakikisha mipango ya Serikali inatekelezwa kikamilifu, hasa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa mkoa wa Pwani.
Wananchi hao wa Mkoa wa Pwani wamehimizwa kuzingatia ushauri huu ili kuimarisha maendeleo yao kupitia viongozi wa Chama cha Mapinduzi.