Na Sophia Kingimali
Serikali imehitimisha zoezi la uokoaji na kufukua kifusi cha jengo la ghorofa tatu lililoporomoka katika Soko la Kimataifa la Kariakoo, tukio ambalo lilisababisha vifo vya watu 29 na wengine 86 kujeruhiwa, huku wawili wakiendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Akizungumza leo, Novemba 26, 2024, Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, amesema miili 29 imeopolewa, lakini miili mitatu haijatambuliwa na bado ipo hospitali ikisubiri taratibu za kitambulisho kufanyika.
“Zoezi la uokoaji limekamilika, na hatua inayofuata ni kushirikiana na wafanyabiashara wa eneo husika kuchambua mali zao zilizookolewa. Kifusi kimehifadhiwa sehemu salama ili kuruhusu hatua nyingine kufanyika,” alisema Makoba.
Aidha, Makoba alieleza kuwa Serikali imewaruhusu wafanyabiashara waliokuwa wamezuiwa kufungua maduka yao karibu na eneo la tukio kurejea katika shughuli zao kama kawaida.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alieleza kuwa hatua za kufunga biashara jirani na eneo la tukio zililenga kutoa nafasi ya kuokoa manusura, kusitiri miili ya marehemu, na kulinda mali za wafanyabiashara dhidi ya wizi.
“Tumefunga kipande cha Mtaa wa Manyema na Mchikichi hadi Congo ili kuruhusu uchunguzi wa majengo jirani na kubaini uimara wake. Hii pia ni fursa kwa wafanyabiashara wadogo kuanza kufikiria mbinu salama za kufanya biashara bila kuziba barabara muhimu za dharura,” alisema Chalamila.
Chalamila aliongeza kuwa tukio hili limetoa funzo kwa wafanyabiashara kuwekeza katika bima za majengo wanayopanga na kuhifadhi mizigo sehemu tofauti na duka ili kupunguza hasara wakati wa majanga.
Jengo hilo lililokuwa mtaa wa Mchikichi na Congo liliporomoka Novemba 16, 2024, majira ya saa tatu asubuhi, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali pamoja na vifo na majeruhi.
Chalamila alibainisha kuwa mmiliki wa jengo hilo anafahamika na kwamba uchunguzi wa kina wa vyombo vya dola utaendelea ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo na hatua stahiki kuchukuliwa.
Hii ni ajali kubwa inayotoa onyo kwa wote kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ujenzi na utunzaji wa mazingira salama ya biashara.