Na Mwandishi wetu, Tanga
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeibuka mshindi wa jumla katika riadha kwa wanawake kwenye mashindano ya SHIMMUTA 2024 yaliyohitimishwa Mkoani Tanga tarehe 24 Novemba, 2024.
Katika mashindano hayo NCAA iliwakilishwa na wanariadha watatu ambapo Juliana Lucas aliibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za mita 200 na mshindi wa pili kwenye mita 100, mshiriki wa pili Ghati Charles Jackson aling’ara kwa kushika nafasi ya pili kwenye mbio za mita 400 na Israel Romayani Moleli akinyakua nafasi ya tatu kwa upande wa wanaume katika mbio za mita 800.
Mashindano ya SHIMMUTA yaliyoshirikisha taasisi 96 yalianza tarehe 10- 24 Novemba, 2024 ambapo yalifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko tarehe 18 Novemba, 2024 na kufungwa rasmi tarehe 24 Novemba, 2024 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo ambapo kaulimbiu ya mashindano hayo ilikuwa “Michezo na Uwajibikaji: Wanamichezo tushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 kwa Uongozi bora na Maendeleo ya Taifa”