Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila, ametangaza kuwa Jiji la Dar es Salaam litakuwa mwenyeji wa tamasha kubwa la bia la mwisho wa mwaka, “Bata la Disemba Carnival,” litakalofanyika kwa mara ya kwanza kuanzia Desemba 6 hadi 8, 2024, katika viwanja vya Leaders Club. Tamasha hili limeandaliwa kwa ushirikiano wa Mkoa wa Dar es Salaam na Kampuni ya Heineken Beverages International.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Chalamila alisema, “Bata la Disemba si sherehe tu; ni taswira ya maendeleo tuliyopiga kama mkoa na taifa. Carnival hii ni sherehe ya uhai wa kiuchumi wa Dar es Salaam na nguvu za kitamaduni.”
Chalamila alifafanua kuwa tamasha hilo litahusisha muziki, chakula, burudani, na bia bora kutoka Heineken. Sherehe hiyo inatarajiwa kuvutia zaidi ya wahudhuriaji 10,000 kutoka Afrika Mashariki, hivyo kukuza uchumi wa ndani na kuunda fursa nyingi kwa biashara ndogo, wasanii, na wajasiriamali.
“Carnival hii itaangazia umaarufu wa Dar es Salaam kama kitovu cha kitamaduni na biashara, huku ikiimarisha mshikamano wa kijamii na furaha miongoni mwa wakazi na wageni,” alisema Chalamila.
Aidha, RC huyo alitangaza kuwa katika sherehe hiyo, mitungi 1,000 ya gesi itagawiwa kwa Mama Lishe na Baba Lishe, hatua ambayo itaongeza mchango wa kijamii wa tukio hilo.
Chalamila alimshukuru Meneja Mkazi wa Heineken Beverages International, Bw. Obabiyi Fagade, kwa imani yao kwa Dar es Salaam na kwa kushirikiana nao kufanikisha tamasha hilo.
“Maono ya Heineken yanalingana na azma yetu ya kuifanya Dar es Salaam kuwa kivutio cha kimataifa kwa matukio makubwa yanayowaunganisha watu katika kusherehekea utamaduni na maendeleo,” alisema.
Kwa upande wake, Bw. Obabiyi Fagade alisema, “Bata la Disemba Carnival” ni zaidi ya burudani; ni nafasi ya kuimarisha mshikamano wa kijamii, kuongeza fursa za kiuchumi, na kukuza sifa ya Tanzania kama kitovu cha utalii na uwekezaji wa kimataifa.”
Carnival hiyo itaangazia maonyesho ya muziki kutoka kwa wasanii wakubwa wa ndani, vyakula vya asili, na fursa za kiuchumi kwa biashara za eneo hilo. Maelezo zaidi kuhusu ratiba na mauzo ya tiketi yatatangazwa hivi karibuni.
Tamasha hili linaonyesha dhamira ya pamoja kati ya Heineken na Mkoa wa Dar es Salaam ya kuleta maendeleo na mshikamano, huku likiwa ni hatua muhimu kuelekea kukuza utalii na uwekezaji wa kimataifa.