*Bodi ya TAWA yaridhishwa na uboreshaji wa miundombinu ya utalii*
Na Beatus Maganja, Arusha.
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeanza rasmi utekelezaji wa mikakati ya kuiendeleza na kuiandaa Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park iliyopo Mkoani Arusha Kwa ajili ya kupokea wageni wengi zaidi kwa kuongeza mindombinu ya utalii hususani barabara, ujenzi wa mabwawa ya maji Kwa ajili ya wanyamapori na kuondoa mimea vamizi ndani ya eneo hilo.
Hayo yamesemwa leo Novemba 24, 2024 na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Dkt. Simon Mduma katika ziara ya wajumbe wa Bodi hiyo ya kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TAWA ndani ya Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park.
“Hifadhi hii ni mpya ilikabidhiwa takribani mwaka mmoja uliopita na katika mchakato wakuiendeleza na kuiandaa Kwa ajili ya kupokea wageni kulikuwa na umuhimu wa kuongeza barabara kwenye maeneo haya ili wageni watakaokuwa wanatembelea eneo hili wawe na wigo mpana wa kuiona mandhari nzuri sana ya eneo hili lakini vilevile kutoa nafasi kubwa ya kuona vivutio ambavyo vipo kwenye hifadhi hii” amesema Dkt. Mduma
“leo tumezunguka na tumeona maendeleo ya ujenzi wa barabara, ni kazi ambayo inaridhisha, ni nzuri na ratiba ambayo ipo kwa makubaliano kwenye mikataba Kazi ya ujenzi wa barabara inaendelea vizuri sana hilo tumeridhika nalo” ameongeza” Mduma.
Dkt. Mduma amesema kutokana na eneo la Makuyuni kukumbwa na changamoto ya ukame wakati wa kiangazi kiasi cha kusababisha wanyamapori kutoka nje ya hifadhi hiyo na kwenda kwenye makazi.ya watu, Bodi ya TAWA iliona umuhimu wa kujenga bwawa la kukusanyia maji Kwa ajili ya wanyamapori, hivyo Bodi hiyo imefanya ukaguzi wa eneo litakapochimbwa bwawa hilo na kuridhishwa nalo, na hivyo ujenzi wake utaanza hivi karibuni kwakuwa mikataba imekwisha sainiwa tayari Kwa kuanza kazi hiyo.
Kwa upande wake mjumbe wa Bodi hiyo Profesa Suzanne Augustino ameipongeza Menejimenti ya TAWA na watumishi wote Kwa jitihada kubwa wanayoifanya kuboresha mazingira ya Makuyuni Wildlife Park ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi ushauri na maelekezo yanayotolewa na Bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis R. Semfuko.
Aidha Profesa Suzanne ametanabaisha kuwa kutokana na kuendana na kasi ya Rais wa awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa Balozi wa utalii wa nchi yetu na uwekezaji wa miundombinu ya utalii unaofanywa na TAWA, Makuyuni Wildlife Park ya miaka mitano ijayo haitakuwa kama inayoonekana leo badala yake itakuwa Makuyuni yenye mabadiliko makubwa ambayo inafungua njia kwa watalii wengi zaidi lakini pia Makuyuni yenye utofauti mkubwa na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii.
Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini ya TAWA Privatus Kasisi amesema Kitendo cha Serikali kuiamini TAWA na kuikabidhi eneo hilo muhimu kumeipa chachu na nguvu ya kuliendeleza na kulisimamia kwa ukamilifu ili kulifanya liwe bora kwa manufaa ya wakazi wa Mkoa wa Arusha na Taifa Kwa ujumla.
Aidha Kasisi amesisitiza kuwa TAWA itahakikisha inaongeza kasi ya uboreshaji wa miundombinu ya eneo hilo ili kupata watalii wengi na mapato kwa muda mfupi hasa katika mashindano ya AFCON ya mwaka 2027 ambapo Tanzania inatarajia kupokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali na Arusha ni moja ya miji ambayo itapokea wageni hao.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa eneo la Makuyuni Wildlife Park Andrew Kishe amesema miradi yote inayotekelezwa na TAWA ndani ya Hifadhi hiyo inagharimu zaidi TZS Billioni moja ambayo inajumuisha barabara atakazopewa mkandarasi na zile zinazotengenezwa Kwa kutumia vitendea kazi vya taasisi huku akibainisha kuwa barabara zinazofunguliwa zina mrefu wa Kilometa 18.
Vilevile miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa geti kubwa la kisasa la watalii na bwawa la maji Kwa ajili ya wanyamapori ambapo ujenzi wa miradi yote hiyo inatokana na fedha za ndani ya taasisi ya TAWA.