Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Munisi (katikati), akiwa katika picha ya pamoja Maafisa na Watumishi wa Ofisi hiyo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma alipo tembelea banda tarehe 23 Juni, 2026, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Munisi (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa na Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania alipotembelea banda hilo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika tarehe 23 Juni, 2026, Jijini Dodoma.
Na OWM-KAM, Dodoma
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Eveline Munisi amewataka watumishi wa umma nchini kuendeleza utamaduni wa kutoa huduma bora na kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma zinazochochea maendeleo yao.
Dkt. Munisi ametoa rai hiyo baada ya kutembelea na kukagua shughuli zilizotekelezwa na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyohitimishwa Juni 23, 2026, katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Amesema juhudi zilizofanywa na watumishi wa umma pamoja na washiriki wa maonesho hayo zimechangia kwa kiasi kikubwa kusogeza huduma muhimu za Serikali karibu na wananchi na kuwawezesha kupata taarifa sahihi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi na mashirika ya umma.
“Maadhimisho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wananchi kwa kutoa huduma, elimu na kupokea maoni yao kuhusu namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma za umma,” amesema Dkt. Munisi.
Aidha, amepongeza ushiriki wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake kwa kuonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi na kwa wakati, sambamba na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Katika hatua nyingine, Dkt. Munisi amewahimiza wananchi kuendelea kutembelea mabanda ya Ofisi hiyo na taasisi zake katika maonesho na matukio mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ili kupata elimu na taarifa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa.
Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Susan Kimambo amesema kuwa zaidi ya wananchi 320 walitembelea banda la Ofisi hiyo katika kipindi cha maadhimisho hayo na kupata huduma pamoja na elimu kuhusu masuala ya kazi, ajira, ukuzaji ujuzi na mahusiano kazini.
Amesema mwitikio huo unaonesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na umuhimu wa kupata taarifa sahihi zinazowasaidia kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yameendelea kuthibitisha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kuimarisha utoaji wa huduma bora za umma na kujenga jamii yenye uelewa mpana kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali.
