Na Mwandishi Wetu.
Tahadhari imetolewa kwa Wananchi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vitongoji na Vijiji kuwa makini na maneno ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya makundi yenye nia ovu ya kuharibu taswira ya uchaguzi wa amani Nchini.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Novemba 23,Jijini Dar es salaam na Mwanasheria wa porini wa Siasa,Dini,na Ustawi wa Jamii Tanzania, Bw. Mussa Ally Chengula wakati akizungumza na Waandishi wa habari.
Bw. Chengula amesema kuwa suala la uchaguzi wa viongozi wa nafasi mbalimbali katika ngazi za serikali nchini ni miongoni mwa mambo muhimu na utendaji wake unahitaji kuzingatia utii, kulinda, kutetea na kufuata kwa lazima Sheria ,kanuni na taratibu za Nchi.
” Tunapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari ya matumizi ya hekima na busara katika vipindi vyote na wakati wote wa uchaguzi wa viongozi wa wanchi katika nafasi mbalimbali za serikali hususani mwaka huu wa uchaguzi wa serikali za Mitaa,Vitongoji na Vijiji Novemba 27 ,2024,na mwakani katika uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani”amesema Bw. Chengula.
Nakuongeza kuwa” kumejitokeza makundi mbalimbali ya upotoshaji yanayoendelea kwa makusudi kupotosha umma kuwa kulikuwa na mwenendo mbaya katika mchakato mzima wa uandikishaji wa daftari la makazi la wapiga kura za serikali za Mitaa,Vitongoji na Vijiji,pamoja na kuenguliwa kwa makusudi wagombea wa nafasi za ujumbe na uenyekiti wa Vitongoj,Vijiji,na Mitaa wa vyama vya upinzani”.
Aidha Bw.Chengula ametoa ushauri kwa Wananchi,wanasiasa wa chama tawala, vyama vya upinzani,wasomi,wafanyabiashara,makundi maalum,na Taasisi zote nchini, kuwa na umoja katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za Mitaa,Vitongoji na Vijiji.
Aidha amesema kuwa misimamo na matamko yote ya upotoshaji yaliyotolewa na vikundi mbalimbali ikiwemo wanasiasa na baadhi ya taasisi za kidini, kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vipuuzwe na badala yake wananchi wenye sifa za kupiga kura waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi Novemba 27,2024 ili wachague Viongozi watakaowaletea Maendeleo.
Aidha Mwanasheria huyo wa porini wa siasa ,Dini na Ustawi wa Jamii Tanzania, Wananchi wote wenye uzalendo na nchi ya Tanzania,na wapenda amani na maendeleo wasikubali kudanganywa kwa kubaguana kichama,kikanda,kikabila,kisiasa,kijinsi,kidini,na kimuungano.
“Makundi hayo ya kichochezi yameamua kwa makusudi kuisema vibaya serikali ili kuidhoofisha na kuipotezea nguvu ili kutengeneza mwanya wa kuondoa imani ya wananchi dhidi ya serikali na watendaji wake akiwemo raia namba moja kimamlaka mama wa Taifa Dkt,Samia Suluhu Hassan na watendaji wake” amesema Bw.Chengula.