Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Bi Fatma Hamad Rajab akifunguwa Mafunzo ya kuwawezesha Vijana waliomaliza masomo yao huko katika Ukumbi wa Ofisi Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini Wilaya ya Magharibi B.
………………….
Wilaya Magharibi ‘‘B’’. 21.11.2024.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Bi Fatma Hamad Rajab amewataka Vijana waliomaliza elimu ya juu kujiunga na Mabaraza ya Vijana katika Shehia ili wapate fursa mbalimbali zilizopo.
Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mazizini wakati alipokuwa akifunguwa Mafunzo wezeshi kwa Vijana waliomaliza elimu ya juu, Mafunzo ambayo yameandaliwa na Kampuni ya Zanzibar Start up Association.
Ameeleza kuwa kuna Vijana wengi waliomaliza elimu ya juu wapo Mitaani hawana ajira hivyo Mafunzo hayo yatawasaidia kuibua mbinu mbali za kujinyanyua kiuchumi.
Amesema Vijana hao wanaweledi wa kutosha hivyo wasiogope kueleza mahitaji yao ili yafikishwe katika sehemu husika na kuweza kufanyiwa kazi.
“Fursa zipo nyingi lakini bado Vijana hawajaweza kuziibuwa na kuzifikia, Wanangu munapomaliza masomo yenu tu, jiungeni na Mabaraza kwani kuna fursa za kutosha”amesema Katibu huyo.
Aidha ameeleza kuwa Serikali haina uwezo wa kuajiri Vijana wote wanaomaliza masomo na kuwaomba wasibweteke na badala yake wachangamkie fursa zinazopatikana kupitia Mabaraza hayo.
Alibainisha kuwa Mafunzo hayoy atawaongezea uelewa na ubunifu wa kuangalia Mazingira wezeshi katika kufanya Biashara na Ujasiriamali na kuwapatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo Katibu huyo ameiomba Kampuni hiyo kuhakikisha Vijana wanapomaliza Mafunzo wanawapa Vyeti ili waweze kutambulika na kutumia fursa zinapojitokeza.
Mbali na hayo amewataka Vijana kutojiingiza katika Tabia hatarishi ikiwemo Utumiaji wa Dawa za kulevya na Udhalilishaji wa Kijinsia mambo ambayo yanaweza kuathiri mustakbali wa maisha yao ya sasa na baadae.
Kinyume na hayo amewataka Vijana hao kudumisha Amani ya Nchi iliopo sambamba na kudumisha Mila, Silka na Utamaduni wa Mzanzibar.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa Ndg. Yunus Juma Ali amewataka Viongozi kuwashirikisha katika Miradi mbalimbali ya maendeleo ili waweze kujumishwa ipasavyo.
Aidha amewataka Vijana hao kubadili maisha yao kwa kufuata njia sahihi za kujiajiri na kujipatia kipato ili waweze kufikia malengo waliojipangia.
Hata hivyo ameipongeza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kuwasimamia na kubuni mbinu za kuwaletea Maendeleo ya Kiuchumi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Start Up Association Bw. Ikram Soraga amesema Kampuni hiyo ina lengo la kuwalea Vijana na kuwapatia njia na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Mkufunzi kutoka Tanzania Bara Bw. Mohamed Sleiman ameishauri Wizara kuwasaidia vijana wanaopatiwa Mikopo kuanza kupeleka marejesho angalau kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kunusuru kupeleka marejesho kwa Pesa za Mtaji.