IMANI MTUMWA MAELEZO. 21/11/2024.
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imetoa ruzuku kwa Taasisi 12 za Watu wenye ulemavu ili ziweze kujiendesha.
Akitoa Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na miaka 4 ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi huko katika Ukumbi wa ZBC Mnazimmoja amesema hatua hiyo imesaidia kutatua changamoto walizonazo.
Amesema Serikali imeamua kutaoa Mikopo kwa Watu hao ili waweze kuanzisha miradi ya kiuchumi na kuendesha maisha yao ya kila siku.
Aidha amesema jumla ya Visaidizi 1,381 vya Watu wenye Ulemavu vimetolewa kwa Unguja na Pemba.
Amefahamisha Wizara imeanzisha na kusimamia Mfumo wa kuhifadhi Taarifa za Watu wenye Ulemavu ambapo hadi sasa jumla ya Watu hao 8,615 wamesajiliwa kupitia mfumo huo.
Hatahivyo amesema jumla ya Vijana 98 wenye ulemavu wamepatiwa elimu ya Mafunzo ya amali ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Kwa upande wa suala la Mazingira Mhe. Harousi amesema Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamo wa Kwanza inaendelelea kusimamia na kutekeleza Mpango wa Kuirithisha Zanzibar ya Kijani ili Wananchi na Wadau wazidi kupata uelewa wa kuhifadhi Misitu.
Amesema lengo la Mpango huo ni kuhamasisha na kuwawezesha Wananchi na Wadau wa Mazingira kuzidi kufahamu umuhimu wa kupanda Miti na kuitunza kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.
Sambamba na hayo amesema Wizara imeteketeza jumla ya Kilogramu 1,448,913 za Dawa za kulevya, Watuhumiwa 1,177 wamekamatwa wakihusishwa na kesi za Dawa za kulevya ikiwemo Bangi, Heroin, Mirungi, Kokeni, Codeine, Valium, Mandrax, Morphine na Methamphetamine.
Hata hivyo Mhe. Waziri ameongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu kupitia sekta ya Dawa za kulevya jumla ya Kesi 1,155 zilifunguliwa na Kesi 725 zimeshafikishwa Mahakamani kwa hatua za Kisheria.
Mbali na hayo ameshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi kubwa wanazozichukuwa katika kukuza Uchumi na kutangaza fursa za vivutio vya Uwekezaji vilivyopo Nchini