Na Rahma Khamis Maelezo 19/9/2024
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amewataka madereva kwenda mwendo wa wastani wakati wanapoendesha vyombo vya moto ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu huyo, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuendesha kwa usalama, madereva na makonda wa gari za abiria wa mkoa huo, katika ukumbi wa Ofisi ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Othman Ali Maulid, amesema uzowefu unaonesha kuwa mwendo kasi unachangia ajali nyingi za barabarani na kuwataka wadau hao kufuata maelekezo ya mwendo yaliyowekwa katika alama za barabarani ili watumiaji wa barabara wabaki kuwa salama.
Ameeleza kuwa Serikali imeweka miundombinu ya barabara ili kuhakikisha sekta ya usafiri nchini inaimarika na kuwasihi kuitumia miundombinu hiyo kama ilivyokusudiwa pasi na kuathiri watumiaji.
“Tunapoendesha vyombo vyetu kwa mwendo wa wastani itasaidia kupunguza ajali na endapo zitatokea hzaitakua kubwa kama itavyokua ajali ya mwendo kasi.” alisema Mkuu huyo.
Aidha amewataka waliopatiwa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri wa elimu hiyo ili kuiweka Zanzibar katika hali ya usalama kutokana na ajali za barabarani kwa Zanzibar bila ya ajali inawezekana.
Naye Mkuu wa Kituo cha Umahiri cha Kikanda katika Usalama Barabarani, Chuo Cha Taifa Cha Usafishaji (NIT ), Godlisten Msomanje amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha matumizi salama ya barabara katika kuadhimisha wiki ya usalama barabarani.
Alieleza kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo kwa madereva, kufanya utafiti na kutoa ushauri elekezi ili kuhakikisha usalama wa wananchi barabarani unakuwepo muda wote.
Amesema uzowefu unaonesha kuwa tatizo la usalama barabarani ni janga la kitaifa hivyo elimu inahitajika zaidi ili kuondoa tatizo hilo
“tumekuja Zanzibar kutoa elimu dhidi ya usalama barabarani ili kusaidia kuweka usalama wa watumiaji wa barabara.” Alisema mkuu huyo
Akiwasilisha mada ya Sheria na alama za barabarani, Mhandisi Mhonja Roheje, amesema madereva wengi wanaenda kinyume na taratibu na sharia za barabarani ikiwa ni pamoja na kuendesha bila kuwa na leseni ya udereva, kutokagua vyombo vyao kabla ya kuingia barabarani pamoja na kutofuata alama za barabarani.
“Iwapo utakua na leseni lakini unajaza abiria kupitia kiasi bado hujafuata sheria jambo ambalo linahatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara na kuiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusimamia mikakati zaidi ili kukomesha tabia za madereva na makonda wanaofanya makosa hayo.”alisema Mhandisi huyo
Kwa upande wa madereva na makondawaliyopatiwa mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi kwa maslahi ya watumiai wa barabara na Taifa kwa ujumla na kuziomba taasisi husika kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili kutekeleza majukuumu yao kwa ufanisi.
Mafunzo hayo yametolewa na Mamlaka ya Usalama Barabarani Zanzibar kwa kushirikiana na Chuo Cha Usafirishaji Tanzania, ikiwa ni shamrashamra za wiki ya nenda kwa usalama Barabarani.