Na Mwandishi wetu-Baku Azerbaijan
Sekta ya Utalii imeonekana kuwa ni kichocheo kikubwa cha kukabiliana na mbadiliko ya tabia nchi ambayo kwa siku za karibuni limeonekana ni janga na changamoto kubwa inayoikumba duniani kwa sasa.
Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akihutubia mkutano wa mawaziri wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 jijini Baku, Azerbaijan.
Aidha Mhe. Kitandula alisema kuwa Tanzania katika kutekeleza miradi iliyoko kwenye Sekta ya utalii, huwa inatumia taarifa za Tathmini ya mazingira kwa kuwa zinasaidia katika kuhifadhi na kusimamia uhifadhi wa mazingira endelevu kama kanuni na sheria za utalii zinavyoelekeza kabla ya miradi hiyo kuanza kutekelezwa.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa masuala ya uhifadhi yanaendelezwa alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa matumizi bora ya nishati safi ya Kupikia lakini kwa kuhakikisha maeneo mengi yenye misitu iliyohifadhiwa yanaingizwa katika biashara ya hewa ukaa kwa ajili ya Utunzaji wa Mazingira asilia.
Lakini pia alitumia fursa kuelezea kuwa Mhe. Rais amekuwa akiunga mkono juhudi za kuuntangaza vivutio vya utalii kwenye maeneo yenye mazingira asilia na upandaji wa miti, kwani kwa kufanya hivyo imekuwa ni chachu kwa wananchi na wahifadhi kujikita kwa juhudi na weledi katika suala zima la utunzaji wa mazingira.
Mhe. Kitandula anamuwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana katika mkutano 29 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, ambapo mambo kadhaa yamejadiliwa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ili kufikia suluhisho kwa suala hili ambalo linatishia ulimwengu.
Aidha Naibu waziri hakusita kuwakaribisha wahudhuriaji wa mkutano huo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Seringeti na hifadhi ya Eneo la Mamlaka ya Ngorongoro pamoja na mandhari nzuri za Visiwa vya Zanzibar.