Na Mwandishi Wetu, Tanga Mjini
Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ummy Ally Mwalimu amezindua rasmi Ligi ya Mpira wa Miguu Wilaya ya Tanga ambayo inasimamiwa na Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Tanga (TDFA). Ligi hii ya Mpira wa Miguu imepewa jina la TDFA Odo Ummy Cup 2024/2025 ambapo mdhamini mkuu ni Mbunge Ummy Mwalimu.
Katika uzinduzi wa ligi hii, Ummy Mwalimu aligawa vifaa mbalimbali vya michezo vikiwemo seti za jezi kwa vilabu 27 kutoka kata zote za Tanga Mjini na mipira 31. Vilevile, Ummy Mwalimu kama mdhamini wa ligi hii ameahidi kugharamia fedha za uendeshaji wa ligi mwanzo hadi mwisho ambapo michezo 98 inatarajiwa kuchezwa katika viwanja vya Lamore, Tanga Mjini. Pia ameahidi kutoa zawadi kwa washindi wanne katika ligi hii.
Uzinduzi wa ligi hii umeibua furaha kubwa kwa wakazi wa Tanga Mjini ikizingatiwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa chama cha TDFA kupata mdhamini tangu kuanzishwa kwake.
Sanjari na hilo, ligi hii ni mwendelezo wa mkakati wa Mbunge Ummy Mwalimu kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji kwa vijana wa Tanga Mjini ikizingatiwa kuwa michezo sasa si burudani pekee bali pia inasaidia kulinda afya na kupata ajira.