Na Sophia Kingimali
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameielekeza Wizara ya Madini kuhakikisha inasimamia vyama vya wachimbaji wadogo wa madini ili kuhakikisha wanazingatia sera na sheria zilizopo za uchimbaji, na hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Majaliwa alitoa wito huo leo, Novemba 19, 2024, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unaobeba kauli mbiu “Uongezaji Thamani ya Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii.”
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu alieleza kuwa sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi, na serikali inajipanga kuboresha zaidi mazingira ya wachimbaji wadogo. Malengo ya serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, wachimbaji wadogo wanakuwa wachimbaji wa kati ili kuongeza mchango wao katika uchumi wa taifa.
“Niwaelekeze Wizara ya Madini muendelee kusimamia vyama vya wachimbaji madini. Hatua hii itasaidia kukuza na kuimarisha soko la madini nchini na kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” alisema Waziri Mkuu.
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu aliwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya madini, akisisitiza kuwa Tanzania imejipanga vyema kimkakati na ina maeneo mengi yanayofaa kwa uwekezaji.
Akijibu ombi lililotolewa na Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA) kuhusu kupatiwa leseni, Waziri Mkuu alisema serikali tayari imefanya mapitio ya sera na inaendelea na mchakato wa kutoa leseni hizo kwa wachimbaji wadogo kutumia maeneo yaliyorejeshwa serikalini.
Aidha, aliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo yote ya uchimbaji, akibainisha kuwa Tanzania sasa ina uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha.
MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA MADINI
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini yamechochewa na uongozi bora wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alibainisha kuwa serikali imeongeza bajeti ya sekta hiyo kutoka Shilingi bilioni 89 hadi bilioni 231 ili kuimarisha zaidi sekta hiyo.
“Rais Dkt. Samia ametoa maelekezo ya mashine mbili za uchorongaji kupelekwa kwa wanawake wachimbaji ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kwa ufanisi,” alisema Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde alieleza kuwa sera mpya ya kuongeza thamani ya madini inalenga kutoa ajira kwa vijana wengi na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.
Mkutano huu wa kimataifa umeleta fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya madini, wawekezaji, na serikali, huku ukilenga kuendeleza rasilimali za madini kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.