Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka kumsaka Jennifer Jovin (Niffer), anayesemekana kuendesha zoezi la kukusanya michango bila kibali kufuatia ajali ya jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo.
Akizungumza leo wakati wa zoezi la kuaga kitaifa miili ya watu 16 waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea Novemba 16, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema zoezi la kukusanya michango bila kibali ni kinyume cha sheria na ni wizi wa pesa za Watanzania.
“Nitumie nafasi hii kuwaonya wote wanaotumia fursa ya tukio hili kukusanya michango ya watu bila kibali. Jeshi la Polisi linapaswa kuwatafuta wote wanaofanya zoezi hili, maana huo ni wizi. Jennifer Jovin kama ananisikia, naamtaka ajisalimishe mwenyewe kituo cha polisi kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wadau mbalimbali na wananchi walioguswa na tukio hili kutoa michango yao kupitia akaunti maalum ya maafa iliyopo Benki Kuu ya Tanzania, badala ya kutumia njia zisizo rasmi.
Waziri Mkuu pia aliwaasa wananchi kuwa makini na watu wanaotumia majanga kujinufaisha binafsi, akisisitiza umuhimu wa kuwachukulia hatua kali wote wanaojihusisha na vitendo vya aina hiyo.