Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu akizungumza na waandishi wa abari akiwemo viongozi wa vyama vya siasa (hawapo pichani),leo kuhusiana na mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.
Viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wakimsikiliza Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Ilemela (hayupo pichani), leo. Picha na Baltazar Mashaka)
…….
NA BALTAZAR MASHAKA,ILEMELA
Manispaa ya Ilemela inaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, ambapo jumla ya wagombea 1,798 wa vyama mbalimbali vya siasa wakiwemo 171 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamepitishwa kugombea nafasi za uenyekiti na ujumbe wa kamati za mitaa, vitongoji na vijiji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu, uchaguzi huo utashirikisha vyama 15 vya siasa, huku ikiwa na lengo la kuimarisha ushiriki wa wananchi katika michakato ya kisiasa.
Amesema jumla ya wapiga kura 297,230 wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo, sawa na asilimia 98.3 ya lengo la kuandikisha watu 302,329 ambapouchaguzi huo utafanyika Novemba 27, 2024, katika vituo 493 vilivyopo Manispaa ya Ilemela.
Mchakato wa Uandikishaji na Uteuzi wa Wagombea
Mchakato wa uandikishaji na uteuzi wa wagombea ulianza kwa kujiandikisha wapiga kura,jumla ya wapiga kura 297,230 walijiandikisha, kati yao wanawake 148,294 na wanaume 148,936.
Wayayu amesema uandikishaji ulifanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024, katika vituo 198 vya kujiandikisha, na ulifuatiwa na uhakiki wa orodha ya wapiga kura ili kutoa nafasi ya kufanya uhakiki wa taarifa za wapiga kura na majina yasiyostahili.
Amesema awali wagombea 414 wa vyama mbalimbali walichukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi ya uenyekiti katika mitaa 171 ya Manispaa ya Ilemela.
Hata hivyo, wagombea 4 walikataliwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujiandikisha zaidi ya mara moja, kutokufikia umri wa miaka 21 na kutokujiorodhesha kwenye orodha ya wapiga kura.
Aidha, katika mchakato wa kupinga uteuzi,zilipokelewa pingamizi 144, ambapo wagombea 17 walitenguliwa na wengine watatu wa kamati za mitaa walifutwa kutokana na malalamiko ya ufanisi.
Vyama vya Siasa: Uchaguzi kwa Amani na Haki
Viongozi wa vyama vya siasa wamema kua wanaridhika na mchakato wa uchaguzi huo ulivyoendeshwa,ambapo Katibu wa Demokrasia Makini, Wilaya ya Ilemela, Mohamed Msanya, alisema chama chake kimefurahishwa na uteuzi wa wagombea na hakijaona dosari yoyote.
Amesisitiza kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa haki na utahakikisha ushiriki wa wananchi kwa amani, huku akielezea kutokuwepo kwa rushwa katika mchakato wa uteuzi.
Katibu wa DP Wilaya ya Ilemela, Rebecca Samson, ameelezea kuwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi vimeshirikishwa kila hatua na wanauona mchakato huu umefanyika vizuri.
Amewahakikishia wananchi kuwa uchaguzi utafanyika kwa haki na huru, na wanawake wamepata nafasi ya kugombea kwa uwazi na bila hofu.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Kijamii (CCK) Wilaya ya Ilemela, Holela Mabula, amesema kuwa uchaguzi huu unafanyika kwa utulivu na hali ya kisiasa inayosimamiwa kwa mujibu wa maadili na 4R za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kupiga kura bila woga ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Maandalizi ya Kampeni na Taarifa za Uchaguzi
Wayayu ameeleza kuwa vifaa vyote vya uchaguzi tayari vimepokelewa, na kampeni zitaanza rasmi Novemba 20, 2024 huku akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kujitokeza kwenye mikutano ya kampeni ili kuweza kufanya uamuzi bora wa kumchagua kiongozi anayefaa kuongoza mitaa yao.
Aidha,kabla ya kuanza kwa kampeni,viongozi wa dini na wa vyama vya siasa watakutana na msimamizi wa uchaguzi huo ili kuhakikisha unafanyika kwa amani na kwa utulivu.
Wayayu amesisitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 katika Manispaa ya Ilemela ni muhimu kwa kuimarisha demokrasia, na unaonyesha juhudi za vyama mbalimbali vya siasa kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi.
Wakati wa kampeni,viongozi wa vyama mbalimbali wanatarajiwa kutoa sera zao kwa wananchi na kuhamasisha ushiriki wa kura kwa haki, bila hofu na kwa amani.