Simanzi kubwa imetanda mkoani Iringa kufuatia mazishi ya aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, Ndugu Christina Alex Kibiki, aliyeuawa kikatili tarehe 12 Novemba 2024. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha masikitiko makubwa kutokana na tukio hilo, akilaani vikali mauaji hayo na kutoa pole kwa familia ya marehemu pamoja na wanaCCM wote.
Katika hotuba iliyosomwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, wakati wa mazishi yaliyofanyika eneo la Banavanu, Tosamaganga, Rais Samia alisema:
“Nimesikitishwa na kushtushwa sana na tukio hili la kikatili. Tukio hili limeumiza mioyo ya wengi na limeleta simanzi kubwa sio tu kwa familia ya marehemu, bali kwa wanaCCM na wananchi kwa ujumla. Ni jukumu letu sote kuhakikisha matendo ya kikatili kama haya yanakomeshwa mara moja.
Christina Kibiki alipoteza maisha baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana usiku wa tarehe 12 Novemba, nyumbani kwake. Ripoti za awali zinasema marehemu alipigwa risasi na pia kuumizwa vibaya kwa kuvunjwa mikono yote miwili, hali iliyoibua masikitiko na hasira miongoni mwa jamii. Jeshi la Polisi limeahidi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika na kuhakikisha wanachukuliwa hatua za kisheria.
Akihutubia waombolezaji, Balozi Nchimbi alisema:” Tukio hili ni la kutia hofu na linaenda kinyume kabisa na maadili ya jamii yetu. Tunapaswa kulikemea kwa nguvu zote ili kuhakikisha halijirudii tena. Jamii yetu lazima iendelee kuwa mahali salama kwa kila mmoja.”
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba, alieleza kwamba serikali inafanya juhudi za hali ya juu kupitia vyombo vya dola ili kuhakikisha haki inatendeka.
“Tumepokea ushirikiano mkubwa kutoka mikoa jirani na makao makuu ya polisi. Uchunguzi unaendelea kwa kina, na mara tutakapokamilisha, tutatoa taarifa rasmi kwa uwazi na kwa wakati.”
Aidha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Ndugu Daudi Yasin, alionyesha imani kwa juhudi za serikali akisema:
“Tunaamini wahusika watachukuliwa hatua za kisheria. CCM itaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha haki inapatikana.”
Mazishi ya marehemu Kibiki yalitanguliwa na misa maalum iliyofanyika katika Kanisa la Romani Katoliki, Tosamaganga, ambapo Padri Ernest Magelanga aliongoza ibada ya kumuaga marehemu. Katika ibada hiyo, Padri Magelanga alisisitiza umuhimu wa kudumisha mshikamano na kusimamia haki katika jamii.
Kifo cha Christina Kibiki ni pigo kubwa kwa familia yake, wanaCCM, na taifa kwa ujumla. Simanzi ya tukio hili inapaswa kuwa mwito wa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya kikatili ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu nchini.
Marehemu amezikwa kwa heshima kubwa, huku familia na jamii wakihimiza uchunguzi wa tukio hili ufanyike kwa haraka na kwa haki.