Jitihada za walimu katika ufundishaji na wazazi kupeleka chakula kwa watoto shuleni kumechangia kupandisha ufaulu kwa wanafunzi na kuifanya Halmashauri ya wilaya ya Njombe kutoa zawadi kwa shule na baadhi ya walimu.
Katika Mkutano wa baraza la madiwani Mwalimu Charles Meshack Ofisa elimu Sekondari Halmashauri ya wilaya ya Njombe amesema jitihada za pamoja kati ya walimu na wazazi kumefanikisha kupata ufaulu huo na hivyo Halmashauri imetoa zawadi ya shilingi milioni 1.4 kwa walimu waliofanya vizuri katika masomo ya Kemia,Uchumi na Kiswahili.
Mwalimu Patrick Kiyule toka Ninga Sekondari na Sister Sarapia Mmanda toka Collegine Sekondari wamesema juhudi ushirikiano na ushiriki wa wazazi ndio siri ya mafanikio ya kupanda kwa taaluma.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe Vasco Mgunda amepongeza jitihada za walimu na wazazi katika ufaulu huo na kwamba kazi kubwa inapaswa kuendelea ili kupandisha zaidi taaluma.
Baadhi ya madiwani akiwemo Javan Ngumbuke wamewataka walimu kuendelea kuongeza juhudi huku suala la upungufu wa walimu likitakiwa kufanyiwa kazi.
Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeendelea kupandisha ufaulu mwaka hadi mwaka kwani awali ufaulu ulikuwa chini.