*Rais Samia kuufungua
*Kuhudhuriwa na Wageni Zaidi ya 1,500
*Kupambwa na Hafla Maalum ya “Usiku wa Madini”
Dar es Salaam,
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unatarajiwa kuongeza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini hapa nchini sambamba na kuweka msingi thabiti wa ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini, na kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha watanzania kiuchumi na kijamii.
Amesema hayo leo Novemba 14, 2024 wakati akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya Mkutano wa 6 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini Tanzania, unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, Mkutano huo unaoongozwa na Kaulimbiu ya “Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii” unatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki muhimu Zaidi ya 1,500 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali duniani na kwamba ni jukwaa muhimu kwa wadau wa madini kubadilishana uzoefu, maarifa, na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuongeza tija katika Sekta ya Madini, maendeleo ya taifa na uchumi kwa ujumla.
“Mkutano huu ni jukwaa la kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana maarifa, ujuzi na kuangazia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hii inayokua kwa kasi. Pia, unatoa nafasi kwa washiriki kujifunza kuhusu Sera na mikakati mipya ya serikali, kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na madini, na kushuhudia teknolojia mpya na ubunifu unaoweza kuleta thamani zaidi katika utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini kupitia mawasilisho na maonesho kwenye mabanda yanayoenda sambamba na mkutano” amesema Mavunde
Mhe. Mavunde amebainisha kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha uongezaji thamani wa madini kama njia ya kuleta faida zaidi za kiuchumi na kijamii kwa Tanzania na dunia kwa ujumla na kusisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhimiza uwekezaji katika viwanda vya kuchakata madini ndani ya nchi ili kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania.
Waziri Mavunde ameongeza kuwa, Mkutano huo utahudhuriwa na Viongozi wa Kimataifa wakiwemo Mawaziri wa kisekta kutoka mataifa ya Afrika, wawakilishi wa Kampuni kubwa za madini duniani, mabalozi 31 wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, pamoja na taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na shughuli za madini kwa kuwa Mkutano huo ni fursa ya kipekee kwa wawekezaji na wafanyabiashara kuangalia nafasi za kuwekeza nchini Tanzania.
Aidha, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia sekta ya madini na kuhakikisha kuwa nchi inanufaika kikamilifu na rasilimali zake.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, Mkutano huo utaambatana na hafla ya “Usiku wa Madini” mnamo tarehe 20 Novemba, 2024, halfla inayohusisha utoaji wa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika ya Sekta ya Madini sambamba na maonesho ya bidhaa za madini, ikiwa ni pamoja na vito vya thamani huku ikionyesha nafasi ya madini katika maisha ya kila siku ya Watanzania.
Mkutano huo, unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 19 Novemba 2024, huku ukitarajiwa kufungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi mnamo tarehe 21 Novemba 2024.