Na Neema Mtuka, Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, ametoa wito kwa wakandarasi wanaosimamia miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Mhe. Makongoro alitoa pongezi kwa utekelezaji mzuri wa ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, akisema miradi hiyo inaendana na viwango vya ubora na inaakisi thamani ya fedha iliyotolewa kwa maendeleo endelevu ya jamii ya Mkoa wa Rukwa na taifa kwa ujumla.
Makongoro alitoa wito huo leo, Novemba 13, 2024, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa uboreshaji miji (TACTIC). Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ametembelea na kukagua ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga, ambao unatarajiwa kukamilika Machi 2025, na pia alikagua ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 13.03, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 60.
Mbali na ukaguzi wa miradi hiyo, Mhe. Makongoro alizungumza na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga, akiwahimiza kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, kwa kuwachagua viongozi wanaowataka.
“Sisi wanarukwa tunahitaji maendeleo, na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea fedha nyingi kwa ajili ya miradi hii ili kufanikisha maendeleo bora. Ninawapongeza wakandarasi wetu kwa kazi nzuri, lakini hakikisheni kuwa miradi hii inakamilika kwa wakati ili malengo ya Serikali yatimie na mji wetu upate sura mpya ya kiuchumi,” alisema Mhe. Makongoro.
Mhandisi wa Manispaa ya Sumbawanga, Ndg. John Myovela, alibainisha kuwa serikali imekusudia kuubadilisha mji wa Sumbawanga kwa kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, ambapo kukamilika kwa miradi hiyo kutachochea maendeleo yenye tija.
Baadhi ya wananchi, wakiwemo madereva Joseph Mwitwa na James Sindani kutoka Mtaa wa Mandela, walitoa shukrani zao kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ujenzi wa barabara za lami ambazo zitarahisisha usafiri na kuinua uchumi wa taifa.