Lilian Mtali Mkurugenzi wa Biashara wateja wadogo, wa Kati na Binafsi Benki ya TCB Julia na Jesse Jackson Afisa Mkuu wa Huduma za Kijigitali na Ubunifu wakizindua huduma ya kidijitali ya TCB Lipa Popote kwa ajili ya kutuma na kupokea miamala kwa wafanya Biashara wadogo, wa Kati na wakubwa uzinduzi ukiofanyika katika makao makuu ya Benki hiyo Millenium Makumbusbo jijini Dar el Salaam Leo Novemba 13, 2024.
……………………
TCB Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeanzisha mpango wa kusaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini kwa kuzindua huduma mpya ya kidijitali inayolenga kurahisisha miamala ya malipo. Mpango huu unalenga kuwawezesha wafanyabiashara kufanya malipo kwa urahisi na kupokea fedha kwa usalama, hatua inayotazamiwa kusaidia katika kukuza uchumi wa taifa.
Katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Biashara kwa Wateja Wadogo na Kati wa TCB, Lilian Mtali, alielezea dhamira ya benki hiyo ya kuwa msaidizi wa maendeleo kwa kutoa suluhisho la malipo linaloitwa “Lipa Popote.” Alisema, kwa kutumia huduma hii, wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) wataweza kupokea malipo moja kwa moja kwenye akaunti zao kupitia namba maalum ya malipo, hali inayowapa urahisi na ulinzi wa kifedha.
“Huduma ya Lipa Popote imebuniwa kwa lengo la kuongeza ujumuishi wa kifedha na kusaidia wafanyabiashara wadogo kufanya miamala kwa ufanisi, popote walipo,” alisema Mtali. Aliongeza kuwa huduma hiyo ni sehemu ya mkakati wa TCB katika kutoa msaada wa kifedha unaolenga kuinua wafanyabiashara wadogo na wa kati, ambao wanachangia pakubwa katika uchumi wa taifa.
TCB pia imetenga kiasi cha shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo na wa kati, huku shilingi bilioni 250 zikielekezwa kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali binafsi. Kwa mujibu wa Mtali, benki hiyo imejipanga kuchangia katika kuinua kiwango cha ujumuishi wa kifedha kwa kutoa huduma bora na rahisi kwa wateja wake.
Ofisa Mkuu wa Huduma za Kidijitali na Ubunifu wa TCB, Jesse Jackson, alisema kuwa mpango huu ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo katika kukuza ubunifu na kuwafikia Watanzania ambao hawajapata fursa za kifedha. Alibainisha kuwa suluhisho hili litabadilisha namna wafanyabiashara wadogo wanavyofanya kazi na kuwasaidia kufikia malengo yao ya kiuchumi kwa urahisi zaidi.