Dar es Salaam, Tanzania – Novemba 12, 2024:
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa shisha wanachanganya bidhaa hiyo na dawa mbalimbali za kulevya, ikiwemo heroin, ili kuongeza ladha na kuleta madhara makubwa kwa watumiaji.
Kamishna Mkuu wa DCEA, Kamishna Aretas Lyimo, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya na baadhi ya watuhumiwa sugu wa biashara hiyo. Lyimo alieleza kuwa uchunguzi uliofanywa mwaka mzima kupitia sampuli mbalimbali za shisha umebaini kuwa kuna maeneo ambako bidhaa hiyo inachanganywa na bangi, heroini, na hashishi bila wahusika kujua.
“Kwa sasa tuko katika utaratibu wa kuhakikisha shisha inakuwa chini ya udhibiti wa mamlaka yetu. Tutakutana na wamiliki wa mabaa yanayouza shisha kwa ajili ya kuwapa elimu, pamoja na kuanza ukaguzi ili kuhakikisha uuzaji wa shisha unadhibitiwa kama ilivyo kwa dawa nyingine za kulevya,” alisema Kamishna Lyimo.
DCEA pia imefanikisha kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya kupitia operesheni zilizofanyika kati ya Oktoba na Novemba 2024. Aidha, mamlaka hiyo imekamata mililita 447 za dawa za tiba zenye asili ya dawa za kulevya na kuteketeza ekari 157 za mashamba ya bangi, pamoja na lita 19.804 za kemikali bashirifu. Operesheni hizo zimewezesha pia kukamatwa kwa watuhumiwa 58.
“Kati ya dawa zilizokamatwa, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja ya hashishi zilipatikana eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa. Uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake, ambao hutumia dawa hizo kupunguza msongo wa mawazo na kwa ajili ya kujistarehesha,” alisema Kamishna Lyimo.
Aliongeza kuwa skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, ambayo inasababisha madhara makubwa kiafya. Kuhusu hashishi, Lyimo alieleza kuwa hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, ambayo huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, DCEA ilifanikiwa kukamata mililita 120 za dawa za tiba aina ya Codein, ambazo zilikuwa zikisafirishwa nje ya nchi. Pia, walipata mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi. Dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika.
“Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya dawa za kulevya. Hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya, ambapo baadhi ya watu hujaribu kutumia dawa za tiba kama mbadala wa dawa za kulevya,” alifafanua Kamishna Lyimo.
Mkoani Dodoma, DCEA imewakamata watuhumiwa wawili; Suleiman Mbaruku Suleiman, maarufu Nyanda, mwenye umri wa miaka 52, na Kimwaga Msobi Lazaro mwenye miaka 37, wakazi wa mtaa wa Kinyali, kata ya Viwandani. Watuhumiwa hao walikutwa na gramu 393 za heroin. Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu.
Kupitia operesheni za kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini. Kamishna Lyimo amepongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa nia yake thabiti ya kuhakikisha tatizo la dawa za kulevya linakomeshwa ili kulinda afya na usalama wa Watanzania.