Na Prisca Libaga Arusha
Benki ya NMB imetoa tena msaada wa vifaa tiba kwa hospitali ya Jeshi la wananchi kanda ya Arusha iliyoko Monduli Mkoani Arusha vyenye thamani ya shilingi milioni tatu.
Vifaa vilivyotolewa katika hospital hiyo ya Jeshi ni pamoja na stendi za dripu, vitanda pamoja na magodoro kwa ajili ya kusaidia wananchi mbalimbali wanaofika katika hospitali hiyo kupata huduma bora kwa urahisi zaidi.
Msaada huo ni mfululizo wa misaada inayoendelea kutolewa ba benki ya NMB nchini katika sekta mbalimbali za afya, Elimu , mazingira na majanga mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kuwa taasisi hiyo imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 5.4 kwa mwaka 2024 kwa ajili ya kuchangia huduma mbalimbali nchini.
“Huu ni mfululizo wa misaada tunayoendelea kusaidia jamii zetu na Leo tumekuja kutoa vifaa hivi kwa hospital hii ya Jeshi kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa Wananchi kufanyika katika hospitali hii” amesema Ladislaus.
Amesema wamefanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa afya bora kama moja ya kipaumbele chao kwa maendeleo ya Taifa lolote duniani.
Amesema Serikali imekuwa ikifanya kwa nafasi kubwa katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wakati na kwa ukaribu hivyo wao kama wadau wa maendeleo wana jukumu la kusaidia kuhakikisha mazingira na miundo mbinu yote ya afya yanapatikana.
“Leo tunagawa vifaa hivi kama sehemu ya kutoa shukrani kwa wananchi wanaotuunga mkono kwa kufanya kazi na kufungua akauti zao kupitia benki yetu ambapo tumetenga asimilia moja ya faida kuhakikisha inawarudia wananchi katika huduma mbalimbali”
Amesema katika kuzidi kusogeza huduma kwa wateja, wamefanikiwa kufungua matawi zaidi ya 234 na kusambaza mashine zaidi ya 700 lakini pia wana mawakala zaidi ya 44,000 nchi nzima ili kutekeleza kauli ya ‘NMB Karibu yako’”Amesema.
“Pia tumeendelea kutoa masuluhisho mbalimbali ya kifedha ikiwemo mikopo ya makundi mbalimbali lakini pia kubuni na kuzindua huduma mbalimbali za kidigitali kusaidia kurahisisha huduma kwa wateja, hivyo tunawakaribisha pia wateja kutoka hapa jeshini kuja kufungua akaunti zenu na kuwa sehemu ya mafanikio haya ya huduma kwa jamii” alisema Baraka.
Akipokea vifaa hivyo, Kamanda wa kikosi, hospitali ya Jeshi Kanda ya Arusha, Luteni Kanali Jichola Jilya Masanja ameshukuru kwa msaada huo kutoka NMB na kusema hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya jeshi na taasisi hiyo ya kifedha.
“Kutupatia vitanda, magodoro, na stendi za dripu zitasaidia watanzania wote wanaohudumiwa hapa kupanua wigo wa huduma na sisi kama wadau tunaahidi kutunza vifaa hivi kwa manufaa ya wengi zaidi na tuaomba mashirikiano yaendelee sio Arusha tu na maeneo mengine wafaidike” amesema Mkuu huyo.