Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi
Katika kuhakikisha matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yanapungUa kama sio kuisha kabisa, Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali ya SOS Children Village limeandaa mafunzo maalumu ya siku mbili kwa Askari wote wa Kata kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi.
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoani humo, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Peter Lusesa ambaye alimwakilisha Kamanda wa Polisi amesema mafunzo hayo yatasaidia kwenda kufikisha jumbe mbalimbali zinazopingana na uhalifu hususani ule wa ukatili wa kijinsia unaojumuisha makosa kama vile ulawiti, ubakaji na vipigo.
Aidha amewataka Askari hao kutumia maarifa pamoja na mbinu mbalimbali watakazopewa katika mafunzo hayo kwenda kufikisha ujumbe kwa jamii kuhakikisha matukio ya ukatili na yale ya mmomonyoko wa maadili yanapungua kama sio kuisha kabisa.
Kwa upande wake mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoani humo Mrakibu wa Polisi Happiness Temu amesema katika mafunzo hayo, wakaguzi hao watajifunza namna ya kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya ukatili, kuwawezesha Askari kata kuelewa umuhimu wao katika kuisaidia jamii kuondoa matukio ya ukatili na kufahamu sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia.
Naye Bwana Godlisten Mlay toka taasisi isiyo ya Kiserikali ya SOS Children Village amewaomba wakaguzi hao kuwa mstari wa mbele kufikisha ujumbe kuhusiana na suala zima la ulinzi na usalama wa mtoto kwani limekua ni changamoto sana katika jamii.
Mnufaika wa mafunzo hayo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Happy Mshana amesema mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi hususani katika kutoa elimu kwa wananchi ambao wanaficha matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.