Jukwaaa Wahariri Tanzania TEF limempongeza na kumshukuru Waziri wa Habari, Mawasiliano na Telnolojia ya Habari Jerry Silaa kwa kuteua bodi ya ithibati inayokwenda kuleta utekelezaji wa sheria ya huduma za habari hatua aliyoichukua baada ya kuingia tu madarakani.
Akizungumza leo Novemba 7,2024 jijini Dar es salaam kwenye ufunguzi wa mkutano Mkuu wa nane wa Jukwaa hilo mwenyekiti wa TEF,Deodatus Balile ametoa shukrani kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, kwa kuchukua hatua ya kuunda Bodi ya Ithibati kwa waandishi wa habari.
Bw. Balile amepongeza juhudi hizo akieleza kuwa bodi hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini, pamoja na kulinda viwango vya kitaaluma na kuleta uwajibikaji zaidi katika tasnia ya habari.
Balile ameishukuru serikali kwa usimamizi bora uliopelekea Tanzania kupanda katika uhuru wa vyombo vya habari duniani hadi kufikia hadi 97 kutoka nafasi ya 143 katika uhuru wa vyombo vya habari duniani.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili ameitaja sheria ya mwaka 2016 ya Huduma za Habari iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 akisema kuna baadhi ya mambo yanapaswa kurekebishwa.
“Changamoto nyingine ni sheria inayomzuia mwekezaji kutoka nje ya nchi kumiliki zaidi ya asilimia 49 ya hisa katika kampuni ya habari kwani suala hilo linafifisha uchumi wa vyombo vya habari nchini,” amesema Balile.
Kwa upande wake Naibu Katibu mkuu wizara ya habari,Mawasiliano na Teknolojia ya habari Nicholaus Mkapa Katika hotuba yake, ametoa rai kwa vyombo vya habari nchini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia mambo muhimu ya weledi katika uandishi lakini pia waandishi kujikita katika habari za kimaendeleo ambayo nchi imefanya.
“Wahariri na waandishi wa habari mnaowajibu wa kudumisha amani kupitia kalamu na sauti zenu. Vilevile mnapaswa kuonesha Watanzania maendeleo yanayofikiwa na Serikali ikiwemo reli ya kisasa ya SGR,the bwawa la umeme la Julius Nyerere na maendeleo mengine ikiwemo miundombinu ambayo serikali inazadi kuiboresha,”Amesema Mkapa.
Akijibu changamoto zingine zilizowasilishwa na TEF, Mkapa amesema suala la umiliki wa wawekezaji wa kigeni ni la kisera na mchakato umeanza huku akiahidi kuwashirikisha.
Aidha amesema wanaendelea kupitia sera ili kuweka mfumo mzuri katika sekta ya habari.
“Tutaendelea kuwashirikisha katika michakato pia, wizara inaendelea kufanyia kazi ripoti ya hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini,” amesema Mkapa.
Naye,Muwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia ukweli na haki ili kulinda amani ya nchi.
“Amani inakuja pale tunaporipoti kwa haki na usawa tunaposhika kalamu zetu, tuzingatie maadili katika kazi zetu za uandishi wa habari,”amesema Mpogolo.
Mkutano huo wa Nane wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) umeanza leo Novemba 7,2024 na unatarajia kuhitimishwa Novemba 9,2024 unakwenda na kauli mbiu isemayo”Weledi kwa Uhimilivu wa Vyombo vya Habari,”