WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Balozi Dk.Pindi Chana akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mkoani Arusha leo.
Kamishna Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo akizungumza kwenye mkutano huo leo mkoani Arusha .
………
Happy Lazaro, Arusha .
WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Balozi Dk.Pindi Chana ameitaka manejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuwathibitisha watumishi wenye sifa ambao wamekaimu nafasi hizo kwa muda mrefu, ili kuongeza ufanisi.
Aidha ameiagiza mamlaka hiyo kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ya Tehama ili kubaini changamoto mbalimbali zinazotokea ndani ya maeneo yao, ikiwemo majanga ya moto badala ya kusubiri kuletewa taarifa.
Aidha Waziri Chana amewataka Wahifadhi hao kuweka nguvu kwenye kuzuia uhalifu, uharibifu, kutoa elimu, mafunzo na kuweka mabango yanayoonekana katika maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa hasa kwa kutumia mbinu na vifaa vya za kisasa.
“Endeleeni kuimarisha ulinzi wa misitu hii kwa kuhakikisha misitu yote inajengwa vituo vya ulinzi hususan sasa na matumizi ya Teknolojia katika ulinzi ambapo changamoto za uhifadhi zinaongezeka, kama kutumia ndege nyuki na satellite” amesisitiza Waziri Chana .
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Waziri Chana wakati wa kufungua mkutano wa tatu wa mwaka wa viongozi na makamanda wa hifadhi za misitu, wenye kauli mbiu ya “TFS 2024, Huduma kwa uadilifu ” ambapo makamanda zaidi ya 200 wameshiriki.
“Watu waliokaimu nafasi mbalimbali mida mrefu na zile zilizo wazi hakikisheni zinajazwa ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji kazi,”amesema.
Amesema umefika sasa wakati kwa wale wanaokaimu nafasi mbalimbali kuidhinishwa, ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi kwa serikali na kusimamia ipasavyo maboresho ya maslahi ya wafanyakazi kwa kuwpandisha vyeo na madaraja.
Amesema ni wakati sasa kwa menejimenti ya TFS kuhakikisha wanaboresha maslahi ya watumishi, kwani hivi sasa TFS imetangaza nafasi za ajira kwa watumishi zaidi ya 265 hivyo wahakikishe wanachagua watumishi bora wanaoendana na kasi ya mabadiliko.
Kuhusu majanga ya moto yanayotokea kwa baadhi ya maenro ya hifadhi za misitu alisema endapo wananchi wakipewa elimu juu ya usafishaji mashamba wataweza kuhifadhi misitu ili kuepuka moto kusambaza kwenye misitu na kuepuka uingizaji mifugo ndani ya hifadhi inayochangia kuharibu mazingira ya hifadhi.
“TFS nendeni mkasimamie sheria na taratibu ikiwemo kushirikiana na serikali za mitaa na vijijini, halmashauri na vikao vya ushauri vya mkoa (RCC) kwa pamoja katika utoaji wa elimu ya kusafisha mashamba, nyakati za kilimo ili kuondoa madhara ya moto kuingia katika maeneo ya hifadhi ya misitu na kuleta hasara,”alisema.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TFS ,Mhandisi Emmanuel Nyanda akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa TFS ,Brigedia Jenerali Dk.Mbaraka Mkeremy amesema bodi imetatua chagamoto za watumishi ukiwemo wenye sifa kupandishwa madaraja.
Pia amesema bodi imesimamia maduhuli ya serikali ambapo hadi Juni mwaka huu bodi hiyo imekusanya Sh.bilioni 166 kwa mwaka wa fedha uliopita, hivyo alisisitiza ubunifu wa masuala mbalimbali kwa sababu ni muhimu katika kuhakikikisha mashaba ya miti na upandaji miti yanaimarika, ikiwemo kuongeza malighafi ya kutosha katika viwanda zaidi ya 8002 vinavyotegemea malighafi ya misitu.
Kamishna Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo amesema lengo la kikao hicho ni kujengeana uwezo wa utendaji kazi, kubadilisha uzoefu, kujadiliana na kushauriana kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za utendaji kazi ili kuimarisha mifumo ya utendaji kazi.
Amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine kikao hicho kitatoa mada kuhusu Intelijensia ya mawazo, fikra za kimkakati, kujenga uwezo wa kuongoza, usimamizi wa sekta ya misitu , mbinu za uongozi, usimamizi wa sera na sekta ya ufugaji nyuki, changamoto na mwelekeo wake.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Washiriki takribani 240 ikijumuisha Viongozi wa Kanda zote Saba za TFS pamoja na Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya TFS, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Deusdedit Bwoyo, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, Menejimenti ya TFS, Makamanda wa Kanda na Wahifadhi Wakuu wa Mashamba na Wilaya wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).