Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi akihutubia wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa Uchumi wa Buluu kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Arusha Novemba 4,2024.
Baadhi ya viongozi na wadau mbalimbali walioshiriki kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa Uchumi wa Buluu kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Arusha Novemba 4,2024.
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa Uchumi wa Buluu kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Arusha Novemba 4,2024.
………………
Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi imeweka mikakati ya kuhakikisha rasilimali za Uchumi wa Buluu zinatumika kwa ufanisi ili kukuza uchumi wa Taifa kwa maendeleo endelevu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa Uchumi wa Buluu kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kilichofanyika Arusha Novemba 4,2024, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema katika kufanikisha hilo Juni, 2024 ilizinduliwa Sera ya Taifa Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu (2024 – 2034).
Amesema mpango kazi huu ni nyenzo muhimu itakayotumika kutekeleza malengo, mikakati na shabaha zilizoainishwa katika Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu kwa kipindi cha 2024/25 hadi 2025/26.
Bw. Mitawi ameongeza anaamini uandaaji wa mipango ya utekelezaji wa shughuli za uchumi wa buluu kwa vipindi vya mwaka 2024/25 na 2025/26 utawezesha kutekeleza malengo, mikakati na shabaha zilizoainishwa kwenye Sera ya Taifa Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na mkakati wake ili kuleta tija na maslahi mapana kwa nchi.
“Tanzania ina utajiri wa rasilimali katika maji bahari na maji baridi zinazojumuisha Kilomita za mraba 64,000 za maji ya kitaifa katika bahari, na Kilomita za mraba 223,000 za Ukanda Maalumu wa Uchumi wa Bahari.
Shughuli za Uchumi wa Buluu hapa nchini zinatekelezwa na Sekta za Uvuvi, Nishati, Uchukuzi, Maliasili na Utalii, Maji, Umwagiliaji, Madini, Uhifadhi wa Mazingira, Uwekezaji, Viwanda na Biashara.” Amesema Bw. Mitawi.
Aidha, Serikali imeweka nyenzo mbalimbali za Kisera na Kisheria ambapo pamoja na mambo mengine imeweka utaratibu wa usimamizi na uratibu wa shughuli za Uchumi wa Buluu katika sekta husika.
Mwaka 2023, mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Sera na Sheria za sekta zenye mnasaba wa Uchumi wa Buluu ni pamoja na kuzalisha tani 513,802.47 za mazao ya uvuvi yenye thamani ya Shilingi trilioni 3.5.
Mazao hayo yanayojumuisha tani 479,976.62 kutoka uvuvi wa maji ya asili (uvuvi katika maji baridi ukichangia asilimia 85 na maji bahari asilimia 15) na tani 33,825.85 kutoka ukuzaji viumbe maji zinazojumuisha ufugaji wa samaki, kilimo cha Mwani, Nyasi bahari na ufugaji wa Matango bahari, kugunduliwa kwa gesi asilia takribani futi 3 za ujazo Trilioni 57.54.
Kati ya hizo, futi za ujazo Trilioni 47.13 zinapatikana kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi, kuongezeka kwa idadi ya meli za kitalii kufikia meli nane (8) zilizosafirisha jumla ya watalii 965 kutoka nchi mbalimbali kuja nchini.
“Mafanikio mengine ni pamoja na kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka wastani wa asilimia 58 mwaka 2018 na kufikia wastani wa asilimia 77 mwaka 2023.”
Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na mambo mengine ina jukumu la kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera, mikakati, mipango na programu za Uchumi wa Buluu kama ilivyoainishwa katika Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya Mwaka 2024 na Mkakati wa utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Bw. Amon Manyanya amesema wataendelea kushirikia na serikali pamoja na wadau mbalimbali ili kuona mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Buluu yanafanikiwa zaidi.