Na Sophia Kingimali.Dar es salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM ) Profesa William Anangisye amesema kuna umuhimu wa elimu ya miliki ubunifu kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini kwani elimu hiyo itasaidia kulinda na kufanya bunifu zinazofanywa kuwa na faida kwani bunifu hizo ni biashara.
Hayo ameyasema leo Novemba 4,2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua mafunzo yaliyotolewa kwa wakufunzi wa maswala ya miliki ubunifu kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambapo mafunzo hayo yaliandaliwa na Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) kwa kushirikiana na African Intellectual Property Organization Academy (ARIPO) pamoja World Intellectual Property Organization (WIPO)
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kutaka kuona tafiti zinazofanywa ziwe miliki bunifu zitakazogeuzwa kuwa bidhaa .
Ameongeza kuwa mafunzo hayo wana uhakika yatawapa uelewa wa kulinda miliki bunifu zao wanazozibuni.
“ Miliki bunifu inatoka sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye tafiti zinazofanywa kwenye hiki chuo chetu,”amesema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema wameungana na WIPO na ARIPO kwenye kutoa mafunzo kwa walimu, wataalam na majaji ili waweze kusambaza elimu hiyo kwa watu wengine na hata kuitumia katika utendaji wao wa kazi.
Nyaisa amesema usambazaji wa elimu hiyo itasaidia jamii kujua kuwa miliki bunifu ni ajira na ni utajiri mkubwa.
“Miliki bunifu ni ajira,utajiri na ni bidhaa adimu ambayo wanakuwa nayo watu wachache hivyo uelimishwaji huu unaotolewa utasaidia wale wote wenye miliki bunifu zao kuweza kuzitunza na kuziongezea ubora,”amesema.
Amesema zipo bunifu zenye sifa lakini wamiliki wa bunifu hizo hadi hivi sasa hawajui wazipeleke wapi kwa ajili ya kuzirasimisha.
“Elimu hii inayotolewa itasaidia hata wale wenye miliki bunifu ambazo hazina sifa tunamatumaini zitaboreshwa na zitakuwa bora.
“Ndio maana tumeona tuwaombe wenzetu wa WIPO watoe mafunzo na watakaofundishwa wakatoe elimu kwa wengine na elimu iendelee kusambaa,”amesema.
Kwa upande wake wakala wa usajili wa biashara na amali Zanzibar Mohamed Alli maalim amesema elimu hiyo ni muhimu kuendelea kutolewa kwani itasaidia kulinda na kuhifadhi bunifu kwa ajili ya kuzifanyia biashara kwa manufaa yao binafsi lakini pia kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Nchi zilizoshiriki mafunzo hayo ni Kenya, Uganda, Rwanda,Boswana na Malawi lengo likiwa nchi za Afrika ziweze kupata elimu ya miliki bunifu kwa lengo la kusaidia jamii.