Takdir Ali. Maelezo.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Siti Abasi Ali amewataka wanandoa kustahamiliana na kuvumiliana ili kunusuru ndoa kuvunjika na kuleta athari kwa Watoto.
Ameyasema hayo huko katika Ukumbi wa Polisi Ziwani Mkoa wa Mjini Magharibi wakati wa mahafali ya Wanafunzi wa Maandalizi ya Skuli ya High view iliopo Chukwani Wilaya ya Magharibi B.
Amesema Wazazi wanapoachana wanaoathirika zaidi ni Watoto kwa kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu na malezi bora.
Aidha amewataka Wazazi kuwekeza zaidi elimu kwa Watoto wao ili waweze kuwa Viongozi wazuri wa hapo baadae na kuzisaidia familia zao.
Mbali na hayo amewataka Wazazi kuwa makini katika kufuatilia nyenendo za Watoto wao ili kuwakinga na vitendo viovu ikiwemo Ukatili, Udhalilishaji na Ubakaji.
Hata hivyo amewakumbusha Wazazi na Walezi kushirikiana na Waalimu wao ili Watoto wao waweze kupata elimu bora na kufikia malengo yaliokusudiwa.
Hata hivyo amewaomba Wamiliki wa Skuli kutoa vipao mbele kwa Watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo Watoto wenye ulemavu na Mayatima ili waweze kupata haki yao ya elimu kama Watoto wengine.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya High view Ali Khamis Ali amewaomba Wazazi na Walezi kulipia ada kwa wakati ili kuepusha Changamoto zinazoweza kujitokeza na kurudisha nyuma maendeleo ya Watoto wao.
Hata hivyo amesema tokea kuanzishwa Skuli hiyo wameweza kupata mafanikiao makubwa ikiwemo kuongezeka idadi ya Wanafunzi, kupata nafasi ya kwanza kwa miaka 3 mfululizo kwa Wanafunzi wa kidato cha sita Zanzibar na kuwa miongozi mwa Skuli 17 bora Tanzania.
Nao Wazazi na Walezi wa High view, wameupongeza Uongozi na Waalimu wa Skuli hiyo kwa kusomesha kwa bidii jambo ambalo limepelekea Watoto wao kufanya vizuri katika Mitihani yao ya Taifa.
Hata hivyo wameawomba kuzidisha juhudi za kutoa elimu kwa Watoto wao sambamba na kuwaelimisha dhana nzima ya Udhalilishaji na Utumiaji wa Dawa za kulevya ili Wanafunzi waweze kujikinga na kubaki salama.
Skuli ya High view, iliopo Chukwani Wilaya ya Magharibi B, imeanzishwa mwaka 2000 ikiwa na Wanafunzi 187 ambapo kwa sasa ina jumla ya Wanafunzi 1735.