Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameongoza maadhimisho ya Siku ya Lishe Duniani, ambayo kiwilaya yamefantika katika viwanja vya Shule ya Msingi Majohe, huku akitoa maelekezo kuwa utoaji wa chakula shuleni ni lazima.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, jijini Dar es Salaam, DC Mpogolo, ameelekeza chakula kutolewa shuleni kuwa ni jambo lazima hivyo kuzitaka kamati za shule, maofisa elimu kata na watendaji kusimamia utekelezaji.
Amesema, wakuu wa shule kamati za shule na maofisa elimu kuweka mikakati bora ya matumizi ya chakula shuleni.
Ametaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wataalamu wa afya na lishe kuongeza elimu ya lishe hususan kuwepo siku maalumu ya lishe shuleni.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya pia amesisitiza auanzishwaji wa klabu za lishe shuleni.
Ameeleza klabu hizo zitasaidia kutoa elimu ya lishe na kusimamia maadili.
DC Mpogolo, pia aliwataka wanaume kuhakikisha wanaacha fedha ya kutosha ya matumizi katika familia zao na kuepuka matumizi makubwa katika masuala ya starehe.
Ameeleza, wapo wanaume ambao huacha fedha zisizotosheleza familia kula mlo kamili hivyo kufanya watoto kukosa lishe bora.
Amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya pamoja na kuwa kinara wa lishe.
Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Hamza, amesema jiji hilo limepunguzs udumavu kutoka asilimia 03 hadi 01.