Na Farida Mangube, Morogoro
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, amewasihi wanafunzi waliojiunga na chuo hicho kwa mwaka wa masomo wa 2024/25 kufuata taratibu, sheria, na miongozo iliyowekwa na Wizara ya Elimu ili waweze kufikia malengo yao kielimu.
Prof. Chibunda alitoa wito huo wakati wa kufunga wiki ya mapokezi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza iliyofanyika katika Kampasi ya Solomon Mahlangu mjini Morogoro. Alisema kuwa Menejimenti ya SUA imejipanga kwa kuweka miundombinu wezeshi ya kujifunza na kufundishia ili kuboresha uzoefu wa wanafunzi katika masomo yao.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Maulid Mwatawala, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia, Prof. Samwel Kabote, alisema SUA ina mazingira bora ya kujifunzia, ikiwemo maktaba iliyo na machapisho mbalimbali ambayo yatawasaidia wanafunzi kupata maarifa ya kina.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, upande wa Mipango, Fedha, na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa, alisisitiza kuwa SUA itaendelea kuboresha miundombinu kupitia mradi wa HEET katika kampasi zake zote. Aliongeza kuwa maboresho hayo yatazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kuhakikisha mazingira ya kujifunzia ni jumuishi na rafiki kwa wote.
Aidha, Prof. Muhairwa aliwasihi wanafunzi wanaonufaika na mikopo kutembelea ofisi za mikopo mara wanapokutana na changamoto zozote za kifedha ili kupata msaada wa haraka na kuepuka athari zinazoweza kutokea kutokana na kuchelewa kutoa taarifa.
Wanafunzi waliojiunga na SUA, Elisa Andrea na Maliamu Juma Makoka, wameipongeza menejimenti ya chuo kwa maandalizi mazuri ya kuwapokea na kuwasihi wenzao kusoma kwa bidii na kuepuka kushiriki katika makundi yasiyo na tija ambayo yanaweza kuathiri malengo yao ya kielimu.