Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) ameliambia
Bunge kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza na
kutangaza Lugha ya Kiswahili duniani ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha matumizi
ya Lugha hiyo katika Taasisi za Kikanda na Kimataifa na kuhakikisha
inafundishwa kama taaluma ili kuzalisha wakalimani bora.
Mhe. Chumi ametoa kauli
hiyo Bungeni, jijini Dodoma leo tarehe 01 Novemba 2024 alipokuwa akijibu swali
la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hawa Subira Mwaifunga aliyetaka kujua kwa nini
Lugha ya Kiswahili haitumiki kwenye Jukwaa la Wabunge la Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC-PF) kama inavyotumika kwenye Bunge la Afrika (PAP).
Mhe. Chumi ambaye
alizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwenye nafasi hiyo, mwezi Julai
2024, amesema kuwa Tanzania
imeendelea na jitihada mbalimbali za
kukuza Lugha ya Kiswahili na kufanikisha Lugha hiyo kuridhiwa na SADC kama lugha ya kazi katika Mikutano ya
Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo tangu mwaka
2019, huku ikiendelea na jitihada za kukiwezesha Kiswahili kutumika katika
Mikutano ya ngazi ya Makatibu Wakuu na Taasisi nyingine za SADC ikiwemo Jukwaa
la Wabunge la SADC.
Akijibu swali la nyongeza
la Mhe. Mwaifunga, kuhusu changamoto kwa Serikali katika kugharamia wakalimani
ili kukitangaza Kiswahili, Mhe. Chumi amesema kwamba Serikali kupitia ushawishi
wake, imefanikiwa kujenga hoja ya kushirikiana na SADC katika kugharamia
wakalimali na hoja hiyo kukubalika ambapo sasa SADC inagharamia wakalimani katika mikutano yote inayoendelea chini ya
Jumuiaya hiyo.
“Kuhusu wakalimani, ni
kweli kuna gharama kubwa za kugharamia suala zima la ukalimani. Hata hivyo, kwa
ushawishi Serikali imefanikiwa kujenga hoja ili kusudi mzigo huo uweze kubebwa
kwa ushirikiano kati ya Tanzania na SADC na kwa sasa SADC katika mikutano
inayoendelea wamekubali kugharamia wakalimani,” alisema Mhe. Chumi.
Kadhalika ameongeza
kusema, ili lugha iwe rasmi yapo mabadiliko ya kanuni na miongozo yanayotakiwa
kufanyiwa kazi ndani ya SADC na kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika
kuhakikisha kipengele hicho kinafanyiwa marekebisho ili kuifanya Lugha ya
Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika Jumuiya ya SADC.
Aidha, akijibu swali la
nyongeza la Mhe. Anatropia Lwehikila kuhusu mikakati ya Serikali katika kutatua
changamoto ya upatikanaji wa wakalimani kutoka Tanzania, Mhe. Chumi amesema
kuwa, ukalimani ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine na kutoa wito kwa
wadau mbalimbali vikiwemo Vyuo chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia kuwekeza katika kuhakikisha mafunzo ya ukalimani yanatolewa kama
taaluma ili kuwawezesha wakalimani kutoka Tanzania kukidhi vigezo vinavyotakiwa
na kutumiwa katika mikutano mbalimbali duniani.
‘Ukalimani ni taaluma,
kujua Kiswahili na Kiingereza kama lugha haitoshi kukufanya kuwa
mkalimani. Hivyo, natoa wito kwa Vyuo
vyetu nchini chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
kuhakikisha wanatoa mafunzo ya ukalimani kama taaluma ili na sisi tunapokwenda
katika mikutano mbalimbali duniani tukutane na wakalimani ambao ni watanzania’
alisisitiza Mhe. Chumi.
Kadhalika amesema Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara
za Kisekta ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la
Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la
Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) na Balozi za Tanzania imeendelea na jitihada za
kutangaza Kiswahili kama bidhaa kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa
ikiwemo makongamano, mikutano pamoja na kuwa na madawati ya kiswahili kwenye
Balozi za Tanzania na kuzishawishi Balozi zinazowakilisha nchi zao hapa
Tanzania kuwa na madawati ya namna hiyo.
Mhe, Chumi akijibu swali Bungeni |