Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amezindua kampeni ya tamasha la utalii la pili la “Same Utalii Festival,” litakalofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 22 Desemba 2024. Tamasha hili litakalofanyika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, linatarajiwa kuvutia wageni wengi na kuchangia katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mheshimiwa Kasilda alieleza kuwa lengo la tamasha hili ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii nchini kupitia filamu maarufu, Tanzania the Royal Tour. Alisema tamasha hili ni fursa ya kipekee kwa Wilaya ya Same kuvutia uwekezaji mpya na kuongeza ajira kwa wakazi.
Akieleza zaidi, Kasilda alisema kuwa tamasha hili litaangazia utalii wa asili, ikiwemo tamaduni za kabila la Wapare na Wamaasai, ambazo ni sehemu muhimu ya utambulisho wa eneo hilo. Alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi, akisema, “Tamasha lililopita limeibua fursa nyingi za ajira, hasa kwa wamiliki wa hoteli na wajasiriamali. Tunatarajia mafanikio makubwa zaidi mwaka huu.”
Aidha, aliwahimiza wananchi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuendelea na zoezi la uandikishaji wa wapiga kura ili kuimarisha demokrasia.
Wadau wa utalii, wakiwemo viongozi wa hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, walionesha matumaini ya ongezeko kubwa la watalii, wakisema kuwa tangu kuanzishwa kwa tamasha hili, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 7,000 hadi zaidi ya 20,000.
Tamasha la mwaka huu litajumuisha matukio mbalimbali ya utalii, safari ya treni kutoka Dar es Salaam hadi Same, na burudani kutoka kwa wasanii mashuhuri, likilenga kukuza sekta ya utalii katika Wilaya ya Same na kutangaza vivutio vya kipekee vya eneo hilo.
“Same Utalii Festival” inatoa fursa kwa wajasiriamali na jamii nzima kuonyesha utajiri wa utamaduni na vivutio vya asili vilivyopo Same.