Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota, amewaongoza wakazi wa wilaya hiyo kufanya mazoezi leo, Novemba 1, 2024. Mazoezi hayo yameandaliwa kwa lengo la kuhamasisha ushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Kemirembe alisema mazoezi ni sehemu ya kujenga mwili, lakini pia wameyatumia kama njia ya kuhamasisha ushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Alisisitiza kuwa ni muhimu wananchi kuchagua viongozi watakaosaidia kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo, akizingatia kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Nawaomba sana tushiriki vizuri katika zoezi la uandikishaji, na leo ni siku ya urejeshaji fomu. Nawaomba sana nendeni mkachague viongozi watakaomsaidia Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Kemirembe.
Katika hatua nyingine, Lwota alieleza kuwa mazoezi hayo yalikwenda sambamba na tukio la uchomaji nyama lililofanyika katika viwanja vya mnadani Serengeti, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya “Nyama Choma Festival” iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.