Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba akizungumza kwenye mahafali ya tatu ya Chuo Cha Benki hiyo Jijini Mwanza Leo Oktoba 31,2024.
Mkuu wa Chuo Cha Benki Kuu ya Tanzania, Dkt.Nicas Yabu akizungumza na wahitimu wa chuo cha Benki katika mahafali yaliyofanyika Leo Oktoba 31,2024 jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi naye akitia neno katika mahafali hayo.
……………….
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Wahitimu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania wakumbushwa kuwa wabunifu sanjari na kutumia ipasavyo ujuzi na elimu waliyoipata ili waweze kuleta maendeleo yao binafsi,jamii na taifa kwaujumla.
Hayo yamebainishwa Leo Alhamisi Oktoba 31, 2024 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba wakati akizungumza kwenye mahafali ya tatu ya Chuo Cha Benki hiyo Jijini Mwanza.
Amesema Dunia ya sasa inaushindani mkubwa na uhaba wa ajira,hivyo wahitimu wanatakiwa kujiongeza katika kujiajiri na kunufaika na fursa mbalimbali zinazojitokeza.
“Hii ndio maana haswa ya kujifunza kwa kutumia mfumo wa kujifunza wa vitendo (Competency-based) ujuzi huu utawasaidia sana katika kuingia kwenye soko la ajira na kujiajiri”, alisema Tutuba
Alisema wahitimu wanapaswa kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma na kitaalam kutokana na teknolojia,maarifa kubadilika kwa kasi.
“Kuhitimu kwenu siku ya leo kuwe ni chachu na mwanzo wa safari mpya ya kujifunza na kupata maarifa mapya katika maeneo na viwango mbalimbali”, alisema
Akizingumza kwenye mahafali hayo Mkuu wa Chuo Cha Benki Kuu ya Tanzania, Dkt.Nicas Yabu alisema wahitimu wa Stashahada ya uendeshaji na usimamizi wa mabenki ni 40 kati yao wanaume ni 28 sawa na asilimia 70 na wanawake 12 sawa na asilimia 30 huku wahitimu wa Stashahada ya uzamili katika uongozi wa mabenki wakiwa 38.
Dkt.Yabu alizishukuru taasisi za fedha zinazowapokea wanafunzi wao wakati wa mafunzo ya vitendo na hatimae kuwapa ajira.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi alisema watashirikiana kwa ukaribu na wahitimu hao katika shughuli mbalimbali za kijamii.