Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maji wa Taifa, Wakili Haji Mandule akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika leo, Oktoba 31, 2024, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Maji Mhandisi Abdallah Mkufunzi akiongea wakati akifafanua baadhi ya Mambo katika kikao kazi hicho.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri akifafanua baadhi ya Mambo katika kikaokazi hicho.
………………
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maji wa Taifa, Wakili Haji Mandule, amesema dirisha la mikopo kwa mamlaka za maji mijini na vijijini limefunguliwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma za maji nchini.
Alitoa kauli hiyo katika kikao kazi Kazi kilichofanyika leo, Oktoba 31, 2024, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Mandule alibainisha kuwa si mamlaka zote zinazoweza kukidhi vigezo vya mikopo ya kibiashara kwenye mabenki, na kwa sababu hiyo Mfuko wa Maji umeanzishwa ili kutoa suluhisho kwenye changamoto hiyo. Alisema, “Mfuko wa Maji unalenga kuzipa mamlaka hizi uwezo wa kupata mikopo itakayowezesha utekelezaji wa miradi ya maji kwa gharama nafuu.”
Kufikia Julai 2024, Mfuko huo ulikuwa umetoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 5.3, huku maombi ya mikopo ya thamani ya shilingi bilioni 13 yakiwa yanaendelea kuchakatwa.
Ushirikiano na Benki ya Maendeleo Tanzania (TID)
Mandule alisema kuwa Mfuko wa Maji umesaini makubaliano na Benki ya Maendeleo Tanzania (TID) kwa ajili ya kusimamia mchakato wa mikopo. TID inachakata maombi, inakagua miradi inayokusudiwa, na kutoa taarifa kwa Mfuko kuhusu miradi inayokidhi vigezo vya mkopo. “Kigezo kikubwa ni urejeshaji wa pesa hizo ili kupunguza mzigo kwa serikali na kuwezesha miradi mingine kupata ufadhili,” alisema.
Kuongeza Uwezo kwa Mamlaka za Maji
Mfuko wa Maji umeanzisha mpango wa kuwajengea uwezo mamlaka zinazohusika na utoaji huduma za maji kama vile Ruwasa, katika mikoa ya Rukwa, Njombe, Mbeya, Sumbawanga, Shinyanga, Kigoma, Ruvuma, na Morogoro, ili ziweze kuandaa maandiko ya miradi.
Mandule alisema, “Maandiko tunayotoa ni kwa ajili ya kupata fedha kwa utekelezaji wa miradi, ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha za ndani na nje kupitia wadau mbalimbali.”
Miradi ya Kimkakati Inayoendelea
Mandule alieleza kuwa Mfuko wa Maji una miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa chini ya serikali ya awamu ya sita. Alitaja mradi wa Isaka-Kagongwa mkoani Shinyanga, ambao unawanufaisha zaidi ya watu elfu 62, na mradi wa Katoro mkoani Geita uliogharimu shilingi bilioni 2.5 kwa manufaa ya watu laki moja. Pia, mradi wa Kemondo mkoani Bukoba unatekelezwa kupitia fedha za mfuko huo.
Mandule alihimiza jamii kutunza vyanzo vya maji kwa kupanda uoto wa asili ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.
Katika kikao hicho, maafisa kutoka Ruwasa, mamlaka za maji, na mabonde walipatiwa mafunzo ya kuandaa maandiko kwa ajili ya kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya visima na mabonde.